BAADA ya timu yake kushindwa ‘kufanya kweli’ msimu huu wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amesema
atahakikisha wanasajili viungo mahiri katika kipindi kifupi kichacho cha
usajili maarufu dirisha dogo.
Ikiwa chini ya kocha huyo za zamani wa Taifa Stars, Yanga tayari
imeshapoteza mechi mbili msimu huu, sare moja na kushinda nne ikiwa
nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14.
Kabla ya kuondoka nchini kurejea kwao Brazil kwa ajili ya
mapumziko.aximo ambaye Jumamosi kikosi chake kilishinda mechi ya raundi
ya saba 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam, amesema ana orodha ndefu ya viungo ambao kwa sasa
wanahitajika Yanga.
“Tuko nafasi ya tatu katika msimamo kutokana na upungufu kidogo katika
safu yetu ya kiungo. Usajili wetu wa dirisha dogo utajikita katika
kuiongezea nguvu safu hiyo. Yanga ina washambuliaji na mabeki wengi
lakini kuna upungufu katika kiungo,” amesema Maximo.
“Angalia idadi ya magoli tuliyofunga (magoli 9 katika mechi 7), ni wazi
kwamba kuna tatizo kati ya viungo na washambuliaji wangu. Tunahitaji
viungo wanaotengeneza nafasi nyingi za magoli kadri inavyowezekana.

“Siwezi kukutajia wachezaji tunaowataka dirisha dogo, ni masuala yetu ya
ndani hayo. Lakini ninachoweza kukuhakikisha kwa sasa kuna orodha ndefu
ya viungo ambao nimependekeza uongozi uangalie uwezekano wa kuwapata
walau wawili,” amesema zaidi Maximo.
Kiungo Jonas Mkude wa Simba ambaye leo anafanya maamuzi ya kusaini
mkataba mpya wa miaka mitatu katika kikosi hicho cha Mzambia Patrick,
anahusishwa mno na harakati za kukamilisha mipango ya Maximo ndani ya
kikosi cha Yanga.
MSUVA, KIZZA KIKOSI CHA KWANZA
Aidha, raia huyo wa Brazil amekipongeza kikosi chake kwa kuikarisha
Mgambo Shooting huku akiwamwagia sifa wachezaji watokea benchini, winga
Simon Msuva aliyefunga magoli yote na mshambuliaji kutoka Uganda, Hamis
Kizza.
“Msuva alicheza vizuri sana, Kizza pia ameimarika kwa kiasi kikubwa.
Mara nyingi wamekuwa wakianzia benchi lakini ninaona kuna uwezekano
mkubwa wa kuanza katika mechi ijayo (dhidi ya Azam FC Desemba 28),”
ameongeza.
Simon aliyefunga magoli hayo dakika za 74 na 90, aliingia dakika ya 46
kuchukua nafasi ya kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima
‘Fabregas’ wakati Kizza alipishwa na beki wa pembeni Oscar Joshua dakika
saba baada ya saa ya mchezo huku muuaji wa Stand United, Jerryson
Tegete akichukua nafasi ya mshambuliaji kipenzi cha Maximo, Mbrazil
Geilson Santos Santana ‘Jaja’ dakika ya 46.
“Jaja hakucheza vizuri kutokana na kuugua. Kizza aliona udhaifu wa Jaja,
hakika amecheza vizuri lakini timu nzima imecheza vizuri. Niliona kuna
haja ya kupunguza beki mmoja (Joshua) kwa sababu Mgambo walikuwa wazuri
wa kucheza kwa kujilinda na walikuwa pungufu pia,” alisema.
Tangu kutua kwa Maximo mwishoni mwa Juni mwaka huu, Msuva na Kizza
waliokuwa chaguo la kwanza la kocha Mholanzi Hans van der Pluijm
aliyeondoka, wamekuwa wakisugulishwa benchi huku kocha huyo akiwapa
nafasi Wabrazil wenzake Jaja na kiungo Andrey Coutinho anayemtumia kama
winga.
KOCHA MGAMBO
Kocha wa Mgambo Shooting, Bakari Shime amesema kikosi chake kiliponzwa na maamuzi mabovu ya refa Ngole Mwangole kutoka Mbeya.
“Tangu kuanza kwa msimu huu, sijawahi kulaumu maamuzi ya marefa lakini
mwamuzi wa mechi yetu dhidi ya Yanga mmh, niweke wazi hastahili
kuchezesha ligi kama hii. Sijui TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)
watachukua hatua gani maana walikuwapo uwanjani,” amesema Shime.
Ushindi wa Yanga ulichagizwa mno na maamuzi ya ovyo ya refa huyo, ambaye
alionekana wazi kuifinyanga Mgambo JKT hasa alipoinyima penalti,
mshambuliaji wake Malimi Busungu alipokwatuliwa na beki wa pembeni Juma
Abdul ndani ya boksi la wanajangwani dakika ya 63.
Refa huyo aliionea zaidi Mgambo alipoacha kumlima kadi Abdul na
kumwonesha kadi ya njano Busungu kwa madai kwamba alijiangusha. Refa pia
hakuwatendea haki Mgambo katika goli la pili kwani kipa wao alifanyiwa
rafu kabla Msuva hajapiga shuti kwenye lango lililokuwa tupu.
Yanga imepaa hadi nafasi ya tatu ya msimamo walipokuwa Azam FC ambao
wameitoa Coastal Union nafasi ya pili. Azam na Yanga zote zina pointi 13
lakini wanalambalamba wanabebwa na mtiririko wa herufi.