BAADA ya kuonekana kama kutulia kwa malumbano baina ya Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wakili na mdau mkubwa wa soka
nchini, Damas Ndumbaro, aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Ismail Aden
Rage amelichochea tena suala hilo, safari hii bungeni akihoji ukubwa wa
makato na uhalali wa mgawo unaokwenda kwenye mfuko wa Chama cha Soka Dar
es Salaam (DRFA).
Siku chake kabla ya kupigwa kwa mechi ya kwanza ya watani wa jadi
nchini, Simba na Yanga msimu huu, TFF ilitangaza kuanzisha mfuko mpya
‘Jichangie’ kwa lengo la kusaka fedha kwa ajili ya maendeleo ya soka la
vijana nchini ukitaka kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa klabu
kutoka Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Kampuni
ya Azam Media iliyonunua haki za matangazo ya televisheni ya mechi za
Ligi Kuu.
Uamuzi huo ulipingwa vikali na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara (VPL) kupitia wakili Ndumbaro ambaye ni daktari wa sheria.
Malumbano ambayo baadaye yalisababisha TFF imfungie kwa miaka saba
kujihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Huku hali ikionekana kutulia baada ya malumbano ya takriban miezi
miwili, Rage analiibua suala hilo, tena akiwa ndani ya mjengo (bungeni)
mjini Dodoma, ukumbi ambao umejaa watu wenye taaluma mbalimbali na wengi
wao wakiwa ni wanasiasa.
Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisimama bungeni
mjini humo Ijumaa ya wiki juzi na kutaka kama serikali ina habari ya
makato ambayo klabu zinakatwa ni makubwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Juma Nkamia alisema DRFA kinanufaika kwa kupata fedha nyingi za
makato ya mapato ya milangoni katika VPL bila kuwa na kazi yoyote.
Nkamia alisema DRFA wanapata fedha nyingi za mapato ya milangoni ambazo hazijulikani zinakokwenda wala kazi ambayo zinafanyia.
“Lazima tuchukue hatua,” Nkamia alisema huku akikiri makato yanayokatwa
kwa klabu ni makubwa na kueleza kuwa awali alikutana na Bodi ya Ligi Kuu
(TPLB), TFF na wadau wengine wa soka nchini kuangalia namna makato hayo
yatakavyopungua.
“DRFA katika mechi moja wanapata mgawo mara mbili kwenye ile fomu ya
mgawanyo wa mapato… na hawana kazi yoyote wanayoifanya zaidi ya kusubiri
mapato.
“Sasa timu za vijana wanaohangaika ni TFF na serikali… lakini mapato
yale yanayokatwa na makubwa kupita kiasi. Tumezungumza nao kuona njia za
kuyapunguza.
“Leo ni timu kubwa mbili tu ndiyo zinaweza kuingiza mapato mengi… ni
Yanga na Simba , Yanga ikicheza na Ndanda inaingiza mapato mengi sana
kuliko Ndanda ikicheza na Stand United lakini makato bado ni yale yale.”
Makato ya ajabu ajabu, yasiyo na msingi na mengine mengi yanayofanana,
ambayo yanabadilishwa-badilishwa majina tu licha ya kubeba maana moja,
yameendelea kuzikamua hadi tone la mwisho klabu za Ligi Kuu katika
kampeni “nzito” ambayo binafsi ninaona imedhamiria kuhakikisha
haziendelei.
Mathalani, katika mechi iliyopita ya watani wa jadi, Simba na Yanga
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 18,
zilipatikana Sh. milioni 427 lakini zaidi ya Sh. milioni 49 zilikatwa
kinyonyaji na TFF kwenda mfuko mpya wa ‘Jichangie’ jambo ambalo
linapingwa vikali na Ndumbaro ambaye kabla ya kutupwa jela ya soka,
alikuwa mjumbe wa TPLB.
Katika mfuko huo mpya unaoonekana kumuumiza kichwa Rage, TFF ililamba
Sh. milioni 24.77, Yanga walipata Sh. 17,339,700 na DRFA Sh. 7,431,300.
Mgawo mwingine wa mapato hayo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF,
ni Sh. milioni 43.67 ya uwanja, gharama za mchezo Sh. milioni 24.75,
Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) Sh. milioni 23.29, TFF (ikapata mgawo mwingine)
Sh. milioni 17.47, DRFA (nao wakalamba pesa nyingine) Sh. milioni 10.19,
timu mwenyeji, Yanga (ikapata mgawo wa pili) Sh. milioni 100.46, timu
ngeni, Simba ilipata Sh. milioni 71.34, Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) Sh. 65,176,932 wakati Sh. milioni 21.36 ilichukuliwa na CRDB kama
asilimia tano ya gharama za tiketi.
Mambo ya msingi ya kujiuliza hapa ni vipi DRFA itengenezewe mwanya wa
kupata mapato mengi kuliko klabu ilhali haina shughuli yoyote ya maana
inayoifanya zaidi ya kusubiri mapato ya milangoni kama ilivyoelezwa na
Nkamia? TFF wana maslahi yepi na chama hiki?

Shirikisho linaonekana kuiweka kando Ilani ya Uchaguzi ya Rais wake wa
sasa Jamal Malinzi iliyosisitiza kutetea mapato ya klabu na sasa
imeyarudisha makato ya kinyonyaji ambayo kwenye Uwanja wa Taifa yalikuwa
17 kabla ya kufutwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Amos Makala.
Makala, sasa Naibu Waziri wa Maji, alilazimika kutoa tamko la kuyafuta
makato hayo Januari 22, mwaka jana baada ya NIPASHE kuchapisha ripoti
iliyofichua ‘uozo’ uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji wa TFF kwa
kushirikiana na baadhi ya maofisa wa serikali huku baadhi yao wakijiita
Wachina na kulamba Sh. milioni mbili kwa kila mechi iliyochezwa Uwanja
wa Taifa.
Makato hayo yalikuwa: Maandalizi ya uwanja (pitch preparation), Uwanja
(asimilia 10 sasa 15%), Usafi na ulinzi wa uwanja, Ulinzi wa mechi,
Gharama za mchezo, Umeme (Sh. 300,000 kwa kila mechi U/Taifa), Wachina
(stadium technical support) Sh. 2,000,000, Tiketi, Posho ya msimamizi wa
kituo Sh. 120,000, Kamishna wa mechi Sh. 250,000, Waamuzi Sh. 440,000,
Mwamuzi wa akiba, 70,000, Mtathimini wa waamuzi Sh. 254,000 (ilivyokuwa
msimu uliopita), Kamati ya Ligi, FDF, DRFA na VAT.
Licha ya juhudi za wizara yenye dhamana ya michezo nchini kupunguza
makato, vilio vimekuwa vikubwa sasa kwa sababu ni makato mengi mno
yanayoua timu zetu changa ambazo zinahitaji sapoti ya serikali na TFF
lakini suala hili linaonekana kufanywa kinyume na watendaji wa sasa wa
shirikisho.
Miongoni mwa makato yanayochefua ni mgawo wa vyama vya soka vya mikoa
husika hasa, DRFA ambao binafsi sijaona kitu cha maana kilichofanywa na
chama hicho. Ninakumbuka baada ya gazeti hili kuhoji juu ya uhalali wa
makato 17 ya kinyonyaji Uwanja wa Taifa, DRFA walionekana kushtuka na
kuanda semina ya makocha jijini Dar es Salaam.
Makato wanayopewa DRFA ni ya nini na yanakwenda kufanyia kazi gani ikiwa
kwa sasa vyama vya soka vya wilaya za Dar es Salaam (Kifa – Kinondoni,
Tefa – Temeke na IDFA – Ilala) vyote vimeshapewa hadhi ya mikoa na
vinaendesha ligi zao? Hiki ndicho Rage na wadau wa soka nchini wanataka
wafafanuliwe kwa kina.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mwaka juzi kuwa makato
hayo yanawaumiza na kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka klabu kuungana
ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa
maendeleo ya klabu za soka nchini.
Naye Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele alizigeukia klabu kuwa zenyewe
ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa TFF katika kupanga
gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya gharama za mechi
husika, hali ambayo mwishowe huwaacha wakiambulia fedha kidogo mno
kutokana na mapato ya milangoni.
“Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa mzuri. Klabu hazina
umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na malalamiko,” alisema
Kahemele.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema shirikisho
linalazimika kutoa fedha Sh. 200,000 kwa kila mechi inayochezwa kwenye
Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mafuta ya magari ya polisi.
Simba na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa Taifa
kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na serikali iliwapoza kwa
kuahidi kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, inaonekana hakuna juhudi za kulishughulikia suala hilo hivi
karibuni, huku TFF ikianzisha makato mapya ya kinyonyaji baada ya
serikali kuyafuta yaliyokuwa yanaihusu.
Katika ukokotozi wake, Ndumbaro alisema kama utaratibu wa ukataji makato
ya milango utaendelea kama ulivyopangwa na Kamati ya Mashindano ya TFF
kwa kurudisha makato ya kinyonyaji, DRFA itakuwa inalamba fedha nyingi
kuliko klabu za VPL kwa msimu.
Ikumbukwe kuwa marekebisho ya Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2014
yaliyosababisha kuongezwa kwa mfuko mpya wa ‘Jichangie’ yamefanywa na
Kamati ya Mashindano badala ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
TFF, kinyume cha taratibu na Katiba ya shirikisho hilo, hii ikiwa ni
kwa mujibu wa Ndumbaro.