WAKATI jijini Dar es saalam pambano la jumapili la ligi kuu soka Tanzania bara baina ya vinara Azam fc dhidi ya wekundu wa Msimbazi, Simba sc likizidi kuwa gumzo, jijini Mbeya hali ni tofauti kabisa ambapo kila kona ya jiji mashabiki wanazungumzia mechi ya mahasimu wawili, Mbeya City fc na Tanzania Prisons.
Timu hizo zenya makazi yake jijini Mbeya maarufu kama `Jiji la Kijani` zitakutana kwenye mechi huo utakaopigwa uwanja wa CCM kumbukumbu ya Sokoine.
Mbeya City wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kuwalaza Wajelajela mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza mwaka jana.
Kocha msadizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi alisema mchezo huo utakuwa na mvuto wa aina yake kwasababu utazikutanisha timu mbili zilizosimama maeneo tofauti katika msimamo wa ligi kuu msimu huu.
“Sisi tunapigana kuutafuta ubingwa, wao wanapigana kujinasua kushuka daraja. Si kwamba Prisons ni timu mbovu, isipokuwa ndivyo maisha ya soka yalivyo”.
“Wamekosa nafasi ya juu na sasa wanapigania kukwepa kushuka daraja. Lakini mchezo utakuwa mgumu kwasababu wachezaji wa timu zote wanafahamiana vizuri”. Alisema Maka.
Maka aliongeza kuwa wamefanya maandalizi mazuri zaidi na sasa wapo hatua za mwisho wakiwa na matarajio ya kupata pointi tatu muhimu dhidi ya Prisons.
“Tmejiandaa kwa michezo 26 ya ligi kuu. Kila mechi ni muhimu kwetu. Cha msingi mashabiki wetu ambao ni wachezaji wa 12, tunawaomba wajitokeze kwa wingi siku hiyo”. Alisema Maka.
Wakati Mbeya City wakiwa na kumbukumbu ya kushinda 2-0 mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Prisons wanaugulia machungu ya kufungwa mabao 5-0 na Yanga uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam katikati ya wiki.
Katibu mkuu wa Prisons, Inspekta Sadick Jumbe alisema kuwa wamekubali kufungwa na Yanga kwasababu ni timu kubwa yenye uchu wa kutafuta matokeo kwa ajili ya kutetea ubingwa.
“Timu ya Yanga na sisi ilikuwa sawa na ngumu kati ya Tyson dhidi ya Matumla. Hawa wenzetu wanauhitaji ubingwa kwa nguvu zote, hivyo hawana mchezo.. Tumepigwa 5-0. Kuna wenzetu tunaofanana nao, hao tutafia uwanjani”. Alisema Jumbe.
Akizungumzia mchezo wa jumapili, Jumbe alisema wanaenda kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 mzunguko wa kwanza na wakishindwa sana watawafunga Mbeya City 3-0.
“Utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa sana. Sisi tutaingia pale kutafuta pointi tatu kwa nguvu. Mungu bado yupo nasisi. Mgambo wamepoteza na tumebakia nafasi yetu ya 10, lazima tushindane ”.
“Kwanza watu wengi wataingia uwanjani, pili vijana wana ari kubwa. Itakuwa mechi ngumu, lakini ushindi lazima”. Alisema Jumbe.
Pia aliongeza kuwa Mbeya City wasahau kushika nafasi ya pili au ubingwa kwa msimu huu kwasababu nafasi hizo zinapiganiwa na klabu za Yanga na Azam fc.
“Wenzetu wanasema wanataka ubingwa. Tuongee tu ukweli, nafasi ya pili au ya kwanza kwa msimu hu si rahisi kwao. Lakini wakifanikiwa ni jambo jema na sisi tunawaombea wafanikiwe”. Alisema Jumbe.
Ugumu wa mechi hiyo unajengwa katika mazingira ya timu hizi mbili katika msimamo.
Mbeya City wanawania ubingwa wakiwa nafasi ya 3 kwa kujisanyia pointi 42 kibindoni, huku juu yao wakiwemo Yanga wenye pointi 46, na nafasi ya kwanza wapo Azam fc kwa pointi 50.
Prisons wao wanapambana kushuka daraja wakiwa na pointi 22 katika nafasi ya 10.
Hivyo ushindi kwa timu zote una maana kubwa na lazima makocha wajidhatiti kuhakikisha wanafanikiwa kuibuka na pointi tatu.
Faida kubwa kwa Mbeya City ni kujikusanyia mashabiki wengi zaidi ya Prisons jijini Mbeya na nje ya jiji.
Kikosi cha Juma Mwambusi kimekuwa na mvuto kwa mashabiki wengi kutokana na kufanya vizuri zaidi msimu huu ambao ni wakwanza kwao