JESHI LA POLISI MOROGORO LASEMA HALIJAMPIGA RISASI SHEIKH PONDA


clip_image001Jeshi la polisi mkoani Morogoro limekanusha madai ya kuhusika na kumpiga risasi begani, katibu wa jumuiya na taasisi ya kiislamu nchini, sheikh Ponda Issa Ponda, na kwamba iwapo sheikh huyo anaamini kufanyiwa hivyo, ajitokeze na kuthibitisha kauli hizo ambazo zimeendelea kutolewa na wafuasi wake.
Akizungumzia tukio la vurugu zilizojitokeza baada ya kufanyika kwa mhadhara wa baraza la Iddi, lililoandaliwa na wahadhiri wa kiislamu wa mkoa wa Morogoro eneo la Kiwanja cha ndege,na baadaye kuzagaa kwa taarifa kuwa sheikh Ponda amepigwa risasi na kujeruhiwa, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile (Pichani), amesema saa chache kabla ya mhadhara kumalizika, sheikh Ponda  alijitokeza na kuzungumza na wananchi, na baadaye kuondoka na gari, akisindikizwa na kundi la wafuasi wake waliokuwa kwa miguu, lakini polisi walimzuia kwa mbele katika barabara ya Tumbaku, kwa nia ya kutaka kumkamata kutokana na tuhuma za uchochezi katika mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar, jambo lililosababisha wafuasi hao kuwazuia polisi kwa mawe na kusababisha watumie risasi baridi kupiga hewani kuwatawanya.
Kuhusu kushindwa kumkamata sheikh Ponda wakati akiwa jukwaani, Shilogile amesema ilikuwa ni kuepusha vurugu ambazo zingeweza kujitokeza,ambapo mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 3,000.
Wakizungumza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa morogoro,baadhi ya wazazi waliolazwa na watoto katika wadi namba 06, wamesema Jumamosi jioni vurugu kadhaa zilijitokeza baada ya kuwasili kwa majeruhi sheikh Ponda hospitalini hapo,ambapo kabla ya kupata huduma, aliondolewa na watu waliokuwa na pikipiki.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kwa wafuasi wake na waandaaji wa mhadhara huo, zimebainisha kuwa sheikh Ponda anaendelea vyema jijini Dar es Salaam alikopelekwa,baada ya zahanati mbili tofauti alizopelekwa awali kuonekana kukosa huduma zilizomstahili,na alipewa  huduma ya kwanza ya kuongezewa maji na damu akiwa kwenye gari, na baadae kuondolewa risasi mbili anazodaiwa kupigwa kwenye bega.

0 maoni:

Post a Comment

 
Top