NA BARAKA MBOLEMBOLE 
Miaka mitatu iliyopita wakati wa majira ya kiangazi, 2010 kiungo mshambuliaji Mrisho Ngassa aliihama klabu ya Yanga na kutua Azam FC kwa usajili ambao uliwagharimu Azam zaidi ya shillingI za Kitanzania 90 millioni. Ngassa alijiunga Yanga, Juni, 2007 na akatokea kuwa mchezaji kipenzi kwa makocha Dusan Kondic, na baadae Kostadin Papic. Katika siku zake za mwanzo klabuni Yanga, Ngassa hakuweza kupewa nafasi kubwa sana na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mserbia, Militun Micho, na ninakumbuka mchezo wake wa kwanza wa kimataifa alicheza kwa dakika zisizozidi 15 na kutolewa. Ilikuwa ni mapema mwezi februari , 2007 wakati Yanga ikicheza na na timu ya Petro Atletico ya nchini Angola.

Kocha, Micho alimpanga Ngassa katika kikosi cha kwanza ila baada ya robo saa kiungo huyo akaoneka kuzidiwa mambo mengi na wachezaji wa Atletico, na wakati wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Taifa, Micho akamuinua Mkenya, Bernad Mwalala na akaisaidia Yanga kutoka nyuma na kushinda mechi kwa mabao 3-2. Akiwa na kipaji cha kuchezea mpira na kuutambuka kama wafanyavyo Cristiano Ronaldo au Robinho De Souza, Ngassa alikuwa akihaha kila kona ya uwanja kutafuta mipira na kuichezesha timu. Aliweza kuwang’arisha wachezaji wa safu ya mashambulizi, kama Maurice Sunguti, Mwalala, Boniface Ambani na wengine ambao waliisadia Yanga kutwaa ubingwa katika misimu ya 2007/ 08 na kufanya tena hivyo katika msimu wa 2008/ 09 na baada ya kumaliza katika nafasi ya pili msimu wa 2009/ 10, kiungo huyo alijiunga na Azam kwa staili ya ‘ kuweka rekodi ya usajili nchini’.

Akicheza pembeni ya uwanja na kuingia katikati ya uwanja kwa kasi akiwa na mpira, kulimfanya Ngassa kuhesabika miongoni wa wachezaji bora wa nafasi ya kiungo wa mashambulizi, mtoaji mzuri wa pasi za mwisho, mpigaji mzuri wa krosi za mwisho akiwa katika spidi, baadae akaibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania Bara, katika msimu wake wa kwanza akiwa na Azam FC. Alifunga mabao 16 katika michezo isiyozidi 25 katika msimu wa 2010/ 11, japo Azam ilimaliza katika nafasi ileile tu waliyokuwa wameishia msimu wa nyuma yake ( nafasi ya tatu), Ngassa kwa upande wake binafsi alikuwa na mafanikio makubwa. Alithibitisha thamani yake kwa vitendo. Alistahili kuwa mchezaji ghali wa ligi kuu ya Bara, wakati huo.

Katika msimu wake wa pili akiwa na timu ya Azam, mshambuliaji John Bocco akashinda tuzo ya mfungaji bora akiwa na mabao 16, huku Ngassa akimudu kufunga zaidi ya mabao sita kwa msimu mzima. Alitumia muda mwingi wa msimu wa 2011/ 12 akimchezesha Bocco na kumsaidia kufunga, lakini hakuwa Yule tena. Kiwango chake kilianza kushuka na akajikuta akipoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa na baadae akapoteza na namba katika klabu yake. Wakati wa michuano ya Kagame Cup, mara nyingi alikuwa akitokea benchi na alipokuja kuibusu jezi ya Yanga wakati wa mchezo wa nusu fainali dhidi ya timu ya AS Vita, Ngassa akajikuta akivunja mahusiano yake na Azam. Tetesi zikadizi kuwa kiungo huyo alikuwa akiipenda zaidi Yanga na alikuwa akihitaji kurejea katika klabuhiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani.

Azam ikamuuza kwa mkopo kwa timu ya Simba, ingawa mchezaji mwenyewe hakuonesha kuvutiwa na maamuzi hayo. Baadae akasaini mkataba rasmi na timu ya Simba na kupewa million 45 na baadhi ya vitu vya thamini huku pia mshahara wake ukiwa wa kiwango kizuri. Msimu huu, Ngassa amesajiliwa na Yanga, huku akiwa na mkataba wa mwaka zaidi na timu ya Simba. TFF, Shirikisho la Soka nchini, lilimuizinisha Ngassa kuwa mchezaji wa Yanga na kuitaka timu hiyo kuilipa Simba, 45 millioni ili kupata huduma ya Ngassa. Pia mchezaji huyo alifungiwa kucheza katika michezo sita ya mwanzo ya msimu huu, na akaambiwa kuwa ataruhusiwa kucheza endapo pesa hiyo italipwa. Mchezo wa mwisho katika kuitumikia adhabu hiyo ulikuwa ni ule wa kichapo kutoka kwa Azm FC, wikiendi iliyopita. Na Yanga wamesema watamtumia kiungo huyo katika mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shootings siku ya Jumamosi hii.

NI USAJILI MPYA NA WA GHARAMA 
Ngassa alipoondoka Yanga kwa mara ya kwanza, timu hiyo ilikuwa chini ya mwenyekiti Iman Madega, na uamuzi wake huo wa kujiunga na Azam ulivunja mahusiano kati yake na baadhi ya watu ndani ya Yanga na baadae akaambiwa kuwa ‘ Ni mchezaji wa laki moja’ ambaye hakuwa na thamani yoyote ile kwa Yanga. Nafikiri uamuzi wa Ngassa kusaini Azam ulikuja kama kisasi baada ya timu hiyo kumzuia kujiunga na timu moja ya nchini Norway ambayo ilimtaka kwa ada ya kiasi cha dola za kimarekani laki mbili. Yanga walionekana kuathirika sana katika nafasi hiyo ambayo ndiyo inayowapata ubingwa kwa miaka mingi sasa. Ngassa alijiunga na Yanga kumpokea aliyekuwa winga Said Maulid ‘ SMG’, ambaye alihitisha miaka yake saba ya uchezaji klabuni hapo mwaka 2007 na kutimkia nchini Angola kucheza soka la kulipwa kwa muda wa misimu sita. Kuondoka kwa SMG kulitoa nafasi ya Ngassa kuwa ‘ injini ya timu’ na marta zote alikuwa mchezaji muhimu wakati Yanga ikitwaa m,ataji ya ligi kuu mfululizo.

Ngassa hakuwa na ushindani mkubwa sana wa kugombea namba katika kikosi na hata timu ilipojikuta ikisajili wachezaji 11 wa kigeni wakati Fulani timu ikiwa chini ya Kondic bado kiungo huyo aliendelea kuchomoza katika kikosi cha kwanza. Alipokwenda Azam akajikuta akirundikiwa rundo la wachezaji wa nafasi yake nap engine kuinuka kiuchezaji kwa Hamis Mcha kulipoteza Ngassa. Wakati Ngassa akiwa ametumia misimu mitatu nje ya Yanga, akizurura katika klabu za Azam na Simba, HAKUWAHI kushinda taji lolote lile zaidi yua tuzo ya ufungaji bora. Kwa muda wote huo Yanga imetwaa ubingwa mara mbili na Yanga imefanikiwa kushinda mataji mawili, 2010/ 11 na msimu uliopita. Saimo Msuva ametokea kuwa mchezaji bora wa kiungo wa pembeni hasa baada ya kufanya mambo maklubwa msimu ulipita.

Kuna tofauti katika uchezaji wa Msuva na Ngassa, wakati wote wakiwa na uwezo mdogo wa kuzuia, wanaweza kuwa na kasi sawa nap engine Msuva akawa juu kidogo ya Ngasaa kwa kuwa Ngassa amekuwa akicheza ‘ kifadha’ katika miaka miwili iliyopita. Msuva ni kijana hasa kama ilivyo kwa Ngassa ila Msuva anaonekana kuwa na uchu zaidi wa mafanikio kuliko kiungo mwenzake huyo ambaye alianza kucheza ligi kuu mwaka 2006. Inasemekana kuna jengwe kutoka ndani ya wachezaji wenyewe wa Yanga, hawapendi kuona namna Ngassa anavyothaminiwa kupewa kitita kikubwa. Wakati soka letu likipigiwa kelele kuingia katika mfumo wa kulipwa sifikirii kama kuna haja ya mchezaji kuchukia au kumuonea wivu mchezaji mwenzake kwa kuwa tu analipwa kiasi kikubwa cha pesa. Mshahara wa Felix Sunzu ulikuwa ni tatizo kubwa kwa klabu. Kuna wachezaji ambao waluiona million 5.5 alizokuwa akilipwa kwa mwezi ni nyingi sana na hakutakiwa kuwa analipwa kiasi hicho kutokana na huduma aliyokuwa akiitoa uwanjani. Mkataba ni makubaliano ya pande mbili, hivyo mimi sioni tatizo kama kunakuwa na wachezaji wanatumia majina na uwezo wao kuchuma vitita vikubwa vya pesa.

Sitapenda kuona Ngassa akipigiwa pasi za ‘ mgongo’ na wachezaji wenzake wa Yanga, sitapenda kuona vita ya kurushia maneno kutoka kwa baadhi ya wachezaji wenyewe kwa wenyewe kwani hiyo ni tabia mbaya. Kila mtu atakula kutokana na urefu wa kamba yake mwenyewe. Msimchukie Ngassa kwa kuingiza kiasi kikubwa cha pesa, shirikianeni kuipaisha klabu yenu. Ngassa, Msuva, Said Bahanunzi, hawa watauana katika winga ya kulia, kushoto yupo ‘ pass master’ Haruna Niyonzima. Jamani msimpigie Ngassa pasi za mgongoni msaidieni na atawaidieni pia. Hata naye aliwahi kuitwa ' mchezaji wa bei rahisi' 0714 08 43 08

0 maoni:

Post a Comment

 
Top