Na Elius Kambili

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage aliposema hivi karibuni kuwa “Kama serikali imeweza kujenga uwanja wa kisasa (wa taifa) kwa muda wa miaka 50, iweje mimi niweze ndani ya miaka miwili?” alimaanisha uwanja alioahidi kuujenga sasa haiwezekani.

Rage alitoa ahadi hiyo alipoingia madarakani Mei, 2010. Aliahidi kuendeleza mchakato wa ujenzi wa uwanja huo, eneo Bunju, Dar es Salaam.

Lakini kwa kauli hiyo mpya ilimaanisha Simba haiwezi kujenga uwanja wake kwa sasa. Macho na masikio ya wadau wa soka yalielekezwa kwa watani wao Yanga, klabu iliyofikia hatua hata ya kuonyesha michoro ya uwanja na kuunda kamati maalum kwa ajili ya ujenzi huo.

Yanga walikuja na wazo hilo mwaka 2010 kwamba itajenga uwanja wa kisasa katika eneo la Jangwani yalipo makao makuu ya timu hiyo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga.

Novemba mwaka jana klabu hiyo iliingia mkataba wa awali na kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group (T) Limited (BCEG) kuhusu ujenzi wa uwanja wa kisasa.

Katika makubaliano hayo, ujenzi wa uwanja huo ulipangwa kuanza Juni mwaka huu baada ya tathmini mbalimbali kufanyika ikiwezo za kiufundi na kiuchumi. Makubalino hayo ya awali yaliyosainiwa Novemba 23, 2012.

Yanga ilitakiwa kupata na kuwa na eneo la kutosheleza malengo ya mradi, kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi na pia kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi.

Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha. BCEG ikafanya tathmini na kuchora ramani ya ujenzi wa uwanja huo. Kazi hiyo ilikamilika Aprili mwaka huu yaani miezi mitatu kabla ya kuanza kwa ujenzi wa uwanja huo. BCEG ilikabidhi ramani tatu kwa Yanga ili wachague moja tu.

Wakati akikabidhi ramani za ujenzi wa uwanja huo, Meneja Msaidizi wa BCEG, David Zhang Chengwei aliweka wazi kwamba, ni jukumu la Yanga kuamua aina ya uwanja inaouhitaji, kulingana na uwezo wao wa kipesa, ingawa vyote ni vya kisasa.

Gharama za ujenzi wa uwanja A ilielezwa ni dola milioni 50, pamoja na ofisi, ukumbi wa mikutano, maduka, maegesho na sehemu ya mazoezi (gym). Uwanja B gharama zake ni dola milioni 40, huku ule C gharama zikiwa ni dola milioni 30, ingawa vyote vina mahitaji muhimu.

Kwa mujibu wa ramani hizo, Uwanja A ambao ni wa kufunikwa juu, utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 50,000, Uwanja B watazamaji 40,000, na Uwanja C utakaokuwa umefunikwa jukwaa kuu pekee utaingiza watazamaji 30,000 walioketi.

Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa heka 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la ghorofa tatu.

Jengo hilo lilijengwa kwa ufadhili mkubwa wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu. Kwa kutambua udogo wa eneo lake, Novemba mwaka jana klabu hiyo iliandika barua kwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuomba nyongeza ya eneo.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Yanga, ambaye pia mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa uwanja huo, Francis Kifukwe Septemba 30 mwaka huu aliomba msaada kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam juu ya suala hilo baada ya kuona barua hizo hazijajibiwa.

Kifukwe pia alionyesha ramani kwa waandishi wa habari kwa kusema ndani ya eneo la heka tatu la Yanga, kuna kipande cha eneo hilo kilichoingiliwa na wananchi. Wananchi hao wavamizi wanatakiwa kuhama ili kutoa nafasi ya ujenzi huo. Yanga imechagua kujenga uwanja B utakaoweza kubeba watazamaji 40,000.

Ukitazama hapo kuna maswali mengi ambayo majibu yake ni kizungumkuti kwani ukianza na hoja ya kuongeza eneo inaonekana wazi utata utatawala kwani bado wizara haionekani kuwa na jibu zuri kwa Yanga kupewa eneo la ziada kutoka viwanja vya wazi vya Jangawani. Pia kuna ugumu wa kuwaondoa watu wanaodaiwa kuvamia uwanja wa Yanga.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, mamlaka husika ilionekana hazikuwa na taarifa na barua zilizoandikwa na Yanga kuhusu ongezeko la eneo lakini kitendo cha Kifukwe kukataa kusema njia mbadala ya ujenzi huo kama maombi yao yatagonga mwamba ni kama anasema uwanja huo hauwezi kujengwa.

Kifukwe alishindwa kueleza ‘plan B’ ya Yanga wasipopata eneo la nyongeza; pia hakuweka wazi zitakapopatikana dola milioni 40 kwa ujenzi huku tayari kukiwa na taarifa kwamba benki mbalimbali zina wasiwasi wa kukopesha klabu za Simba na Yanga kwa kuogopa kupoteza wateja.

Benki zinaogopa kupoteza wateja endapo Yanga au Simba zitashindwa kulipa mikopo na mali zao kupigwa mnada huku wateja wao wakiwa miongoni mwa wanachama wa klabu hizo.

Pia eneo la Jangwani ni bonde kubwa huku eneo la Yanga likianzia eneo la juu, hivyo tuta linalosemwa na Kifukwe kwamba litawekwa linaweza kuwa la kihistoria Afrika Mashariki na Kati.

0 maoni:

Post a Comment

 
Top