DADA wa Mwenyekiti wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amefariki papo hapo
baada ya gari alilokuwa akiendesha kupasuka tairi ya mbele na kuingia
chini ya daraja baada ya kupinduka na kusababisha watu wawili kufa na
wengine watatu kujeruhiwa vibaya.
Dada huyo, Grace Aikaeli Mbowe,
anayesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 47 hadi 50, alikuwa akiendesha
gari yenye namba T 277 CAJ aina ya Toyota Cresta akiwa na mumewe
aliyefahamika kwa jina la Ibrahim Lukindo (52), wakitokea Jijini Tanga,
walipata ajali hiyo eneo la Kabuku wilayani Handeni.
Kamanda wa polisi mkoani Tanga (ACP)
Costatine Massawe alisema kupitia Ofisa wake wa upelelezi mkoani Tanga,
Bw Aziz Kimata, kwamba ajali hiyo ilitokea majira ya saa 1:30
asubuhi jana katika eneo hilo baada ya gari hilo kupasuka tairi ya mbele
kulia na kisha kuingia chini ya daraja lililokuwepo eneo hilo.
"Ni kweli kuna ajali ilitokea eneo la
Kabuku gari aina ya Cresta lililokuwa likiendeshwa na ndugu
inavyosemekana wa Bw Freeman Mbowe, limepata ajali baada ya kupasuka
tairi la mbele na kuacha barabara na kuingia chini ya daraja .
"Dereva
anayeitwa Grace Aikael Mbowe na mtu anayesemekana ni mumewe anayeitwa
Ibrahim Lukindo, wamefariki na watu watatu waliowachukua wamejeruhiwa,"
alisema RCO Kimata.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja
na Bw Ridhiwani Bakari (29) aliyekuwa na mkewe Zeddy Nzuke (29) raia wa
Kenya aliyekuwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili na miezi minne
aliyefahamika kwa jina la Mariam Ridhiwan ambao kwa sasa wamelazwa
katika hospitali ya Magunga wilayani Korogwe.
RCO Kimata aliyezungumza kwa niaba ya
kamanda huyo wa polisi alisema chanzo cha ajali hiyo inasemekana
kimetokana na kupasuka kwa mpira huo na mwendo kasi wa kawaida na kwamba
majeruhi na maiti zi9mehifadhiwa kwenye hospitali hiyo.
Mwandishi wa habari hizi, aliyefika
kwenye hospitali hiyo na kuzungumza na Ridhiwani pamja na mkewe ambaye
amelazwa wodi namba mbili ya wanawake katika hospitali hiyo, alisema
kwamba ndoto zake za kufanya kazi Dar es salaam zimezimika ghafla
kutokana na kwamba alikuwa aende kupamba kazi ya uofisa ugavi katika
taasisi moja ya fedha ya marehemu Mbowe Jijini Dar es salaam.
"Nilikuwa naenda kupewa kazi na mama
Mbowe katika Institution yake ya Micro-Financial Jijini Dar es salaam,
mimi ni procurement (Mgavi-manunuzi) na ni Mkenya kwetu ni Eastern
Province Kang'undo na nimeolewa na bwana Mtizedi...Lakini sasa ndoto
zangu za kufanya kazi Dar es salaam zimezimika ghafla," alisema Zeddy
akiwa kitandani amelala na mwanwe ambaye alikuwa haongei tangu amefika
katika hospitalini hapo.
Mumewe na mwanamke huyo akizungumzia
ajali hiyo alisema kuwa hakuwa akijua kwani alikuwa amelala dakika tatu
kabla ya kutokea ajali hiyo ambapo alishtukia yeye, mkewe na mwanawe
wametupwa chini kwenye majani wakiwa hawajijui na walikimbizwa katika
hospitali hiyo ya Korogwe
Ridhin ambaye ni mkazi wa Nguvumali
Jijini Tanga, alisema safari yao hiyo ilikuwa ifanyike Jumamosi mchana
lakini kutokana na na kuchelewa kwa wenyeji wao hao, waliondoka Tanga
kwenye hoteli ya Doliphin walikolala majira ya saa 11:00 alifajiri kwa
ajili ya kwenda Jijini Dar es salaam.
Muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo Bi
Nayela Missingo alikiri kuwapokea wagonjwa hao ambapo alisema wanafanya
jitihada za kuwahamishia katika hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar
es salaam mtoto Mariam ambaye amepata majeraha katika kichwa chake na
kwamba tangu afikishe hospilaini hapo hakuwa katika hali nzuri, haongei
walakunyonya.
Bi
Zeddy Nzuke na mtoto wake wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Magunga
wilayani Korogwe baada ya kupata majeraha katika ajali hiyo.
0 maoni:
Post a Comment