UAMUZI wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kumwidhinisha Emmanuel Okwi kuichezea SC Villa ya Uganda umeibua mapya Simba.

Katibu Mkuu wa Simba, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, Evodius Mtawala alisema: “Hatukubali, madai yetu yamebadilika sasa tunadai mambo mawili, tupewe Dola 300,000 halafu watupe na asilimia 20 ya pesa watakayomuuza Okwi kwa SC Villa.”

Simba wameenda mbali zaidi na kudai mpaka Ijumaa wiki hii, Etoile du Sahel itawatambua wao ni nani, kwa kuwa Fifa itakuwa imeshashusha rungu lake dhidi ya timu hiyo ya Tunisia.

Mtawala alisema hawana shida na Okwi wanachohitaji sasa ni fedha zao tu ambazo ukizibadilisha kwa madafu zinakuwa Sh480 milioni.

“Tunataka salio tu, Okwi hawezi kwenda SC Villa bila ya Simba kushirikishwa. Villa wanajisumbua tu kwa kuwa mkataba wetu ambao tumeingia na Etoile du Sahel wakimuuza mchezaji lazima watupe asilimia 20 ya fedha wanayomuuza.”

Fifa imetoa baraka zake kwa Shirikisho la Soka Uganda (Fufa), kumwidhinisha Okwi kuichezea Villa kwa miezi sita, baada ya Fufa kutuma maombi Fifa wakitaka Okwi aruhusiwe kuichezea Villa kwa muda wakati sakata lake likitafutiwa ufumbuzi.

Fifa imelitaka Shirikisho la Soka la Tunisia (FTF), litoe leseni ya uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Okwi kupitia mfumo wa kielektroniki (TMS).

0 maoni:

Post a Comment

 
Top