Na Mwandishi Wetu
MABERE Nyaucho Marando, wakili wa mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ amesema amemaliza kazi ya kuwatetea wafungwa hao waliohukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kuwanajisi watoto 12 waliokuwa wakisoma Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza jijini Dar es Salaam.
Babu Seya (wa pili kulia) na Papii Kocha (wa pili kushoto) wakiwa mahakamani kusikiliza rufaa yao.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Marando alisema kazi aliyokusudia kuifanya ameimaliza, sasa anasubiri majaji waliosikiliza alichokisema ili watoe uamuzi wa mwisho lakini pia anamtegemea Mungu.
“Mimi kazi nimemaliza sasa nawasubiri hao wakubwa (majaji) ili wapime nilichowaambia kwa mujibu wa sheria na kisha watoe uamuzi, lakini pia namtegemea Mungu,” alisema Marando.
Alisema ameiomba Mahakama ya Rufaa Tanzania ifanye marejeo kuhusu hukumu iliyoitoa na ifute ushahidi uliowatia hatiani wateja wake hao na adhabu ya kifungo cha maisha jela wanayoitumikia kwa sasa.
Wakili wa mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, Mabere Marando.
Alipoulizwa alitumia muda gani kuwasilisha hoja zake hizo, Marando alisema takriban dakika 120 mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, wakiongozwa na Jaji Nathalia Kimaro akisaidiana na Jaji Mbarouk Mbarouk na Jaji Salum Massati.
Akiwa mahakamani hapo, Marando alidai kuwa mahakama iliteleza katika kutoa uamuzi uliowatia hatiani na kuwafunga maisha wateja wake na kwamba kuteleza huko kunaonekana waziwazi.
Alifafanua kuwa wakati wakifanya majumuisho ya kesi hiyo, mahakama ilijiridhisha kwamba kulikuwa na makosa katika kupokea ushahidi wa watoto wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo.
Alidai kuwa ushahidi wa watoto hao ulichukuliwa bila ya kufuata taratibu za uchukuaji wa ushahidi wa watoto.
Alieleza kuwa mtoto anayesoma shule kuanzia ya msingi anapotoa ushahidi licha ya tahadhari, ana uwezo wa kutambua zuri na baya na kwamba lazima ushahidi wake uwekwe kwenye kumbukumbu ya maandishi na kwamba usipoonekana ushahidi wote ni batili na unaondolewa.
Babu Seya na Papii Kocha wakiwa na furaha wakati wakitoka katika Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Katika shauri hilo upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka uliwakilishwa na Mawakili Jackson Mlaki, Angaza Mwaipopo, Emakulata Banzi, Joseph Pande na Apimack Mbarouk ambao waliyapinga maombi hayo kuhusu marejeo kwa madai kuwa yamepelekwa mahakamani bila usahihi.
Mahakama hiyo imesema itatoa uamuzi wake siku itakayotangaza.
Babu Seya na Papii Kocha wako jela kwa makosa 10 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo.



Walidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili na Oktoba 2003 eneo la Sinza Kwaremy jijini Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sigirinda Ligomboka ambaye alishitakiwa kwa makosa mawili ya kumsaidia Babu Seya kutenda makosa hayo kwa kuwaruhusu baadhi ya wanafunzi hao kutoka madarasani, aliachiwa huru na Mahakama ya Kisutu.

0 maoni:

Post a Comment

 
Top