Cristiano Ronaldo amesisitiza kwamba hana nia ya kuondoka Real Madrid, akikiri kwamba anafikiria kumaliza maisha yake ya soka ndani ya Santiago Bernabeu.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 28 ambaye alihusishwa sana na kurudi Manchester United mapema mwaka huu, baada ya kusema kwamba hana furaha ndani ya mji mkuu wa Spain, lakini mwishowe akaamua kusaini mkataba mpya utakaomfanya abaki na  Los Blancos mpaka June 2018.

Ronaldo hajutii uamuzi wa kusaini mkataba mpya, akielezea hana mpango kabisa wa kuondoka Madrid.

"Hivi sasa, nahisi nahitaji kumalizia maisha yangu ya soka hapa kwa sababu nina furaha sana," alisema nahodha wa Ureno.

"Napenda kuishi jijini Madrid, kuichezea klabu bora ulimwenguni na sina lingine nilitakalo. Mambo yanapokuwa mazuri, unapokuwa umetulia na kupewa hamasa ya kufanya vizuri zaidi, unakuwa hauna wasiwasi na kitakachotokea mbele.
"Nathaminiwa na kupendwa hapa. Huu ni msimu wangu wa tano hapa. Mwanzoni nilijiona kama sikuwa na nafasi kubwa mioyoni mwa mashabiki, lakini nikagundua kwamba inawezekana ilikuwa mimi ndio ambaye sikuwa sawa. 


"Sasa hivi nina furaha kwa asilimia 100. Ni kama vile ndoto kwenda Bernabeu kila siku, watu wananipenda sana. Nataka kuwa hapa kwa miaka mingi ijayo na kuumaliza mkataba wangu, hakuna klabu nyingine kama Madrid."

Ronaldo ameichezea Madrid katika mechi rasmi 200 tangu alipojiunga nayo akitokea United mwaka  2009.

Wakati huo huo mshambuliaji huyo amesema kwamba haipi sana kipaumbele tuzo ya Ballon d'Or na hajaamua kama atahudhuria sherehe za utoaji tuzo hizo.

"Sikirii sana kuhusu Ballon d'Or. Sijajua kama nitahudhuria sherehe za utoaji tuzo hiyo - sina wazimu juu ya jambo hilo."
 
Top