KIPA Juma Kaseja ametua Yanga kwa mara nyingine baada ya Simba kuachana naye kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Bara, sababu ikatajwa kuwa ameshuka kiwango.

Viongozi wengi wa Simba walipigana vikumbo kuhakikisha sababu za kumuacha Kaseja zinachukua nafasi kubwa kwa jamii kuliko mazuri aliyofanya kwa klabu hiyo kongwe nchini.

Walipoona sababu ya kuwa chini ya kiwango haiingii akilini mwa wadau wa soka hasa mashabiki wa timu hiyo, viongozi hao walibuni kauli nyingine waliyosema kwamba kipa huyo amekuwa na tabia ya kuuza mechi. Hapo walifanikiwa kwani baadhi ya watu hawakutazama aina ya timu waliyokuwa nayo na matokeo wanayopata.

Tazama mechi ya Simba na Yanga ya msimu uliopita, Simba haikuwa na kikosi bora hivyo waliambulia kipigo cha mabao 2-0 Kaseja akiwa langoni. Hakikutazamwa kikosi lakini ikaonekana Kaseja ndiye cha kipigo hicho huku ukweli kuhusu kikosi dhaifu ukikwepeshwa.

Wakati uongozi wa Simba ukipigana vikumbo kuhakikisha unaachana na Kaseja kwa kumuwekea sababu mbalimbali, Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen mara kadhaa amekuwa akiwaaibisha viongozi hao kwani amekuwa akimuita Kaseja katika kikosi chake.


Mijadala ikaanzishwa katika mitandao ya kijamii na hata katika vyombo vya habari kwamba yupi mkweli kati ya Poulsen na viongozi wa Simba.


Kwa kutambua kwamba soka ni kazi yake, Kaseja akaanza kujifua ili kutunza kipaji chake na kweli, leo hii amepata mkataba wa kuitumikia Yanga kwa miaka miwili tena.



POULSEN ALIWAAIBISHA VIONGOZI WANAFIKI
Sababu za kuachwa kwa Kaseja kuhusu uwezo na kuuza mechi zikachagizwa na kisingizio kipya cha kipa huyo kuwa 'babu' yaani mzee ambaye hawezi kuwa na faida katika timu.
Poulsen hakufanyia kazi mizengwe ya viongozi hao iliyosababisha kipa huyo kutupwa nje ya timu huku akiwa na uwezo wake. Pamoja na hali hiyo ya Kaseja kutokuwa na timu, bado Poulsen aliendelea kufanya kazi na kipa huyo na kupata mafanikio.

Na hata matatizo yalipotokea katika kikosi cha Taifa Stars hasa kutopata ushindi, yalikuwa ni matatizo ya jumla ambayo hayakumuhusu Kaseja peke yake. Pamoja na kuitwa kikosini

mara kadhaa akiwa na makipa namba moja wa klabu za Ligi Kuu, kama Ali Mustapha 'Barthez' wa Yanga, Mwadini Ally na Aishi Manula wa Azam, bado Kaseja alikuwa bora na kuwa kipa namba moja.


KIONGOZI HUYU ADUI WA KASEJA
Hata siku moja Kaseja hakuwa anapendwa na viongozi wote wa Simba kutokana labda ya tabia yake ya kudai maslahi yake na wenzake wakati mwingine, hivyo alijikuta akiwa haelewani na viongozi kadhaa wa klabu hiyo.

Japokuwa Kaseja mwenyewe hakuwa tayari kumtaja kiongozi huyo, lakini anafahamika kwamba ni kiongozi huyo ni mjumbe wa kamati ya utendaji (jina tunalo ) ambaye anatajwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Kaseja anaondoka klabuni hapo vyovyote viwavyo.

Kiongozi huyo ndiye aliyeshiriki katika kuhakikisha Kaseja anaondoka na moja kati ya mikakati aliyoiweka ni kuhakikisha anasajiliwa kipa Wilbert Mweta akitokea Toto African ya Mwanza. Lengo la kiongozi huyo ilikuwa ni kuona Mweta anafanya vizuri ili Kaseja aweze kuondoka klabuni hapo.




Huo ulikuwa ni mkakati wa awali ambao Kaseja alikumbana nao na kushinda kwani Mweta hakuweza kuonyesha uwezo wa hali ya juu kumzidi kipa huyo 'mkongwe' katika soka la Tanzania.
Baada ya mkakati huo kushindikana, ndipo zilipoibuka sababu nyingine za Kaseja kushuka kiwango na pia kuwa ni mzee. Wakati viongozi wanasema Kaseja ameshuka kiwango, aliyekuwa kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alikuwa akimtumia, hili lilikuwa tatizo kiuongozi.

MKAKATI WA PILI

Haraka viongozi wa klabu hiyo wakaanza mazungumzo na kipa Abel Dhaira wa Uganda huku wakijua mkataba wa Kaseja unaelekea ukingoni, huyo alisajiliwa na Simba huku akipewa maelekezo ya kuingiza baadhi ya vipengele katika mkataba ikiwemo kile kinachoeleza kuwa anapaswa kuwa kipa namba moja katika timu.
Pia Dhaira aliwekewa mazingira ya kuwa kipa anayelipwa zaidi katika klabu hiyo ili uongozi uone kwamba hakuna haja ya kuwa na mtu kama Kaseja wakati tayari ina kipa mwingine.
Hakika mkakati huu ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa na Kaseja akawa nje ya Simba hadi leo hii.

KASEJA ANAJUA ANACHOFANYA
 

Tofauti na wachezaji wengine, Kaseja mara nyingi amekuwa akipenda kufanya mazoezi binafsi kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo jambo linalomtofautisha na makipa wengine wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Huyu yupo mstari wa mbele kudai haki zake na za wachezaji wenzake pale inapobidi ndiyo maana anakuwa adui wa viongozi walioingia katika soka kwa ajili ya kunyonya wachezaji.
  
SIMBA WAUMBUKA 
Huku ikitegemea Dhaira atafuta aibu ya kutokuwa na Kaseja, ndani ya muda mfupi uwezo wa kipa huyo ulipungua na kuzua hofu ndani ya klabu hiyo kongwe nchini. Haraka benchi

la ufundi la Simba likamtupa benchi Dhaira na kumpa nafasi kipa chipukizi Abuu Hashimu.
Kutokana na mabadiliko hayo ya ghafla lango la Simba halikuwa makini hadi kuiacha timu hiyo ikishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu.  


IWEJE AUZE MECHI HALAFU WAMSAJILI.
 
Hata siku moja, Yanga hawawezi kuwa wajina kumsajili mchezaji iliyekuwa ikimtumia katika kununua mechi za Simba ili awe kipa wao namba moja. Hizi ni propaganda zilizopitiliza.
Japokuwa viongozi wa Simba hawaitaja klabu iliyokuwa ikinunua mechi za Simba kupitia kwa Kaseja, lakini wachambuzi wa mambo wanaamini klabu hiyo ni Yanga kwa asilimia 70 huku Azam ikipewa chache sana.

Leo hii Kaseja kasajiliwa na Yanga, ina maana Yanga itakuwa tayari kuwa na kipa muuza mechi ambaye walikuwa wanamtumia?  Kokote kule duniani huwa hakuna kitu kama hicho.
 

0 maoni:

Post a Comment

 
Top