Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAPENZI wa soka nchini wameombwa kujitokeza kwa wingi kuomba kadi za uanachama katika klabu ya Ashanti United yenye makazi yake maeneo ya Ilala, jijini Dar es salaam.

Afisa habari wa Ashanti, Marijani Rajab ameuambia mtandao huu kuwa mwenye nia ya kujiunga na timu hiyo ya wananchi au ya kijamii afike ofisi zao zilizopo maeneo ya Ilala.

“Tupo Ilala, ofisi zetu zinatazamana na jengo la Mwalimu House, ni jengo dogo na chini yake kuna ofisi za DAWASCO au fika Ilala sokoni kwa wauza mitumba, muulize mtu yeyote ofisi za Ashanti, bila shaka atakuonesha, ni rahisi sana”. Alisema Marijan.
Marijan aliongeza kuwa katika kadi zao wanatumia picha za kidijitali ambazo wanapiga wao na gharama ya picha hizo  ikiwa ni pamoja na ada ya awali ya kadi hiyo ni shilingi za Kitanzania elfu kumi na moja  tu (11,000/=) na baada ya dakika kumi  kadi yenye ubora wa juu inatolewa.
“Kadi zetu ni za kisasa zaidi, karibuni wote wanaotaka mapinduzi ya soka la Tanzania. Njoo uungane na watanzania wenzako wenye mapenzi na Ashanti Unted. Timu hii ni ya Kihistoria, ina malengo makubwa ya kufuta ufalme wa Simba na Yanga”. Alisema Marijan.
Afisa habari huyo alifafanua kuwa kama kuna mtu anataka kujiunga na matawi, Ashanti wana tawi kubwa linaloitwa Napoli na mtu yeyote anaweza kwenda hapo  kumuuliza katibu kuhusu taratibu zao ambazo ni rahisi sana.
Marijan aliwatoa hofu watu kuwa vigezo na masharti ni vilevile kwa mujibu wa sheria, mtu awe na umri wa miaka 18, awe na akili timamu na vingine ambavyo sheria na katiba inaruhusu.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa watanzania kujiunga na timu hii ya kijamii ili kutoa `Ubepari` wa Simba na Yanga.
“Timu zinazoonekana kuwa na mwelekeo wa kuondoa ufalme wa Simba na Yanga ni zile za makampuni binafsi. Lakini Ashanti ni timu ya kijamii, ina uhusiano mkubwa na wananchi. Ina malengo ya kuuondoa Ukurwa na Udoto wa Simba na Yanga”.

 
Top