Ofa ya Manchester United ambayo inaaminika kuwa kiasi cha £37m, imekubaliwa na klabu ya Chelsea kwa ajili ya usajili kiungo wa kihispania Juan Mata.
Kiungo mwenye miaka 25 atafanyiwa vipimo vya afya leo Alhamisi kabla ya kukamilisha usajili wake wa kujiunga na mabingwa hao wa EPL.
Mata anategemewa kusaini mkataba wa miaka minne na nusu wa kuwepo Old Trafford.
Mhispania huyo, ambaye alikuwa mchezaji bora wa Chelsea katika misimu miwili iliyopita, aliwaaga wachezaji wenzie jana Jumatano katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea - Cobham.
United hata hivyo wameendelea kukaa kimya kuhusu uthibitisho wa dili hilo huku kocha wa klabu hiyo akikataa kujibu swali kumhusu Mata baada ya kipigo kutoka kwa Sunderland katika nusu fainali ya kombe la ligi.
Waandishi wa habari walikuwa wametaarifiwa kabla ya mkutano wa baada ya mechi kwamba Moyes atajibu maswali kuhusu mechi tu na baadae walipojaribu kumuuliza kuhusu Mata, kocha huyo mscotish alijibu: "Hatusemi kitu chochote kuhusu hilo jambo."
Ikiwa uhamisho huo utakamilika basi United watakuwa wamevunja rekodi ya ada ya usajili ya klabu hiyo - walilipa kiasi cha £30.75m kwa Spurs kwa ajili ya kumsaini Dimitar Berbatov September 2008.