Emmanuel Okwi, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, ameruhusiwa kuichezea klabu yake ya Yanga na Shirikisho la Soka Ulimwenguni, FIFA. Awali, Okwi alizuiwa kuiwakilisha Yanga na kamati ya sheri na hadhi ya wachezaji ilimsimamisha kwa muda mchezaji huyo kuitumikia, Yanga ili kuulizia, FIFA uhalali wa mchezaji huyo kuichezea Yanga. Majuzi, FIFA, wametoa taarifa kuwa Okwi anaweza kuichezea klabu yake mpya kwa sasa, ila wakisema kuwa sheria itachukua mkondo wake endapo mchezaji huyo ataonekana ni tatizo katika ' ukungu' uliotawala katika usajili wake.
JE, OKWI ANAPASWA KUICHEZEA YANGA MSIMU HUU?.
Ndiyo, kama walivyosema, FIFA, Okwi amepewa ruhusa ila kitendo cha Yanga kumtumia kinaweza kuwaletea matatizo katika siku za mbele, endapo itabainika Okwi alifanya udanganyifu katika klabu yake ya awali, Etoile du Salehe ya Tunisia, ambao bado wanasisitiza kuwa mchezo huyo ni mali yao na hawajui alipo tangu, mwezi Mei, 2013.
TFF KATIKA MTEGO?
Wao wenyewe tayari wamesema kuwa watakaa na kulipitia suala hilo katika mtazamo wa ndani ya nchi. Shirikisho hilo la soka Nchini, limesema kuwa ruhusa ambayo FIFA, wametoa katika matumizi ya Okwi kwa wakati huu , wameikubali. Umejaribu kujiuliza itakuwaje siku za mbele mchezaji huyo akionekana ni tatizo?
Itavuruga mpira wa Tanzania, hasa endapo Yanga watakuwa wamemtumia katika michezo ya ligi kuu.Labda kwa vile kuna kumbukumbu kubwa mbaya kuhusu uvunjifu wa kanani na sheria mbalimbali katika soka la Tanzania, Yanga wakamtumia kwa kigezo cha kutumia udhaifu huo hata kama itakuja kugundulika kuwa mchezaji huyo ni ' batili kwao'. Ila, sheria iliwafunga katika suala la kumcheza mchezaji hasiyetakiwa katika mchezo, wakati wa mchezo dhidi ya Coastal Union, misimu miwili iliyopita. Walipoteza ushindi katika mchezo mgumu, kisa ilikuwa kumchezesha Nadir Haroub aliyekuwa na adhabu. Ni tofauti na suala hili la Okwi, ila wakati mwingine ni lazima tahadhari ichukuliwe mapema.
TFF, kusema kuwa watalitazama vizuri suala hili kwa ndani ya nchi kutokana na matatizo ambayo yanaweza kuja kutokea katika soka la Tanzania, endapo Okwi atacheza michezo yote ya timu yake ya Yanga na kuisaidia kushinda. Na baadae ikagundulika kuwa mchezaji huyo alikiuka mambo mengi na kuingia mitini bila taarifa, Yanga itakuwa katika nafasi gani?. Je, sheria ikishikilia mkondo wake itamaanisha nini?. Je, itakuwaje kuhusu matokeo yake?. Kiushabiki, Okwi ataanza kuitumikia Yanga haraka sana, ila kwa manufaa ya soka la Tanzania, ni lazima jambo hili lichunguzwe kwa kina kabla mchezaji huyo hajaanza kuichezea Yanga katika ligi ya ndani.
Wammchezeshe tu, katika michuano ya kimataifa kama wanahitaji kufanya ujinga wa kufikiri kimantiki. Ni kweli, tupo tayari kuvuruga mpira wa Tanzania kwa makosa ya mchezaji wa ng'ambo?. Huwezi kuona athari zake kwa sasa, sababu wote tumekuwa tukisukumwa mtazamo wa ' tambo na majisifu', wale mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiwapiga vijembe mashabiki wa Simba, baada ya kupewa ruhusa ya angalizo kumtumia Okwi. WAmejitahidi kuweka hisia zao zote kwa Mganda huyo huku nao wakiwasukuma viongozi wao, ' kuwa kama noma na iwe noma, Okwi aichezee timu yao'. Na, acheze sasa. Ila wasije kuwatumpia lawama viongozi wao siku wakiambiwa kuwa kutokana na matumizi ya mchezaji huyo katika michezo ya ligi kuu, nafasi ya Yanga ni hii…..
UNAYAKUMBUKA, YA JAMAL MALINZI NA VICTOR COSTA?
Yanga walimsaini, Victor Costa kutoka Simba bila ruhusa ya klabu yake. Baadaye Jamal Malinzi, rai wa sasa wa TFF, akiwa kiongozi wa juu wa klabu yake ya Yanga. Aliingia uwanjani na Victor Costa na mchezaji huyo alikuwa amevaa jezi namba tano, yenye jina la DEWJI. Nini kilikuja kutokea?. Costa aliishia kuoneshwa kwa mashabiki wa mashabiki wa timu hiyo waliokuwa katika michuano ya MAPINDUZI CUP, huko Zanzibar na aliporudi Dar es Salaam, akaonekana katika mazoezi ya Simba akiwa na jezi namba tano, yenye jina la MALINZI. Ilimaanisha nini?
Tambo za viongozi wa juu wa klabu za Simba na Yanga, Kassim Dewji kwa upande wa Simna, na Malinzi kwa upande wa Yanga. Ulikuwa ni wakati ambao hata viongozi wa juu wa mpira wa Tanzania walikuwa wakifanya kazi yao kwa mapenzi ya klabu zao. Je, tunapaswa kuishi katika dunia yenye fikra kama hizo hadi wakati huu?. Suala la Okwi, ni tofauti na lile la Costa, na lipo mbali na lile na Nadir. ILA, Malinzi anaweza kutumia historia ya adhabu aliyoipata katika utawala wake Yanga hasa baada ya kuwaadaa mashabiki wa timu yake kwa kuwadanganya kuhusu usajili wa Costa, pia anaweza kuchukulia adhabu ambayo TFF, waliisimamia wakati Yanga walipomtumia, Nadir walikatwa pointi na kumaliza katika nafasi ya tatu.
Msimamo wangu kuhusu suala hili upo palepale, kuwa bado hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu suala la uhamisho wa Okwi. Hila muda bado umebaki kidogo tu ili jibu hili kufumbuliwa kwa uhakika. Wenzentu hawazungumzi, Etoile wapo kimya, Fifa wametoa ruhusa ya angalizo, caf wamemruhusu, TFF, wanatafakari. Duuh! Huyu, Okwi ni zaidi ya wachezaji wote Tanzania. ILA, asifikie hatua ya kuharibu soka la Tanzania katika siku za mbele. CAF, ni wajanja waliitega TP Mezembe na kuiondoa kimizengwe, miaka mitatu iliyopita wapotoa ruhusa kwa mchezaji hasiye halali. Wakairudisha mashindanoni, W. Casablanca, ambayo iliitoa Simba na kufika hadi fainali na kufungwa na Esperance.
Subiri baada ya gemu ya Yanga na wale Waarabu. Nguvu iendane na fikra pia, mapenzi kila mtu anayo. Kwa suala la Okwi, Simba ipo karibu pia. Hila kwa sasa haliwahusu. Naisubiri jezi namba 25 ya Yanga kwa hamu kubwa. Okwi, ni mtihani au mtego kwa utawala wa Malinzi?. Tusubiri tuone kwa kuwa uchunguzi wa kitaalamu unaendelea, hivi ile miezi sita ya fifa inamalizika lini?. Okwi, mwenyewe kafunga mdomo, je anatambua kosa lake?. Au, hapendi kuzungumzia mambo yaliyopita?. Unakumbuka ila makala, ' Yanga wamemnunua wapi Emmanuel Okwi?', sasa nauliza, MMEIFIKIRIA RUHUSA YA ANGALIZO KUTOKA FIFA KUHUSU OKWI? Ata, macho yanapenda kutazama vitu vizuri, ila vitu vibaya pia huonekana.