Na Baraka Mbolembole 

Bao lililofungwa na kiungo- mshambuliaji, Richard Peter dakika kumi kabla ya kumalizika kwa mchezo. Lilitosha kuwapa sare ya kufungana mabao 2-2 timu ya Mbeya City. City walipata sare hiyo dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa, Oktoba mwaka uliopita katika mchezo wa duru la kwanza. Timu hizo zitapambana tena wikendi hii katika mchezo wa marejeano jijini, Mbeya.

City wametoka kupata ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita, wakati Simba imetoka kulala kwa timu ya Mgambo JKT. Simba wanaonekana kuwa na safu kali ya mashambulizi, kwani baada ya Yanga SC iliyofunga mabao 34, Simba ndiyo wanafuatia wakiwa wamefunga mabao 32 katika michezo 17. City wanaonekana kutokuwa na makali sana katika kufunga mabao ila safu yao ya ulinzi ikiwa moja safu ngumu katika ligi. Wamefunga mabao 22, na wameruhusu mabao 13. Wanaweza kuisumbua Simba na kuiangamiza kwa kuwa timu hiyo ya Dar es Salaam, imekuwa si imara sana katika ngome.

   SIMBA INAWEZA KUIFUNGA CITY?

Ni vigumu, ila inaweza kuwa rahisi kama watajipanga vizuri. Hakuna timu ambayo imeweza kuifunga City katika uwanja wake wa nyumbani msimu huu. Lakini, timu hiyo imekuwa ikiruhusu mabao uwanjani hapo na kuna timu zilikaribia kuondoka na ushindi ila zikashindwa kuhimiri presha ya timu hiyo na kujikuta zikiondoka na sare au vipigo. Ikiwa na kumbumbuku mbaya katika uwanja wa Sokoine, Simba inaweza kujipanga na kwenda kushinda kama walivyofanya dhidi ya Tanzania Prisons, miaka mitano iliyopita wakati bao la David Naftal lilipowapatia ushindi wa kwanza dhidi ya timu hiyo ya Magereza katika kipindi cha miaka 11.

Mwenyekiti wa Simba, Mh. Ismail Aden Rage tayari ametoa tambo kuwa watakwenda Mbeya kuchukua pointi zote tatu. Simba imezidiwa pointi tatu na timu hiyo ya kocha Juma Mwambusi, na tayari wamejibiwa kuwa hawatishi. Mtibwa ilipata bao la kuongoza katika mchezo uliopita dhidi ya City ila wakajikuta wakichapwa mabao 2-1. City itakuwa ikimkaribisha kikosini kiungo wake mahiri, Steven Mazanda, pia watakuwa na mshambuliaji wao mwenye nguvu Paul Nongwa, Morgan Yeya ' ticha', Hassan Mwasipili. Simba inaweza kushinda Mbeya kama alivyodai Rage, ila timu hiyo ya Mbeya ni kali sana na inayohitaji uvumilivu wa mchezo kutoka kwa wachezaji wao.

  CITY NI TIMU KALI

Waliweza kuthibitisha hilo walipotoka nyuma ya mabao 2-0 hadi kutengeneza sare ya 2-2 katika mchezo wa awali kati ya timu hizo. Awali, waliweza kusawazisha dhidi ya Yanga na walitia fora waliposawazisha mara tatu dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Chamanzi, na kupata sare ya mabao 3-3. Hiyo inaonesha dhahiri kuwa timu hiyo ni imara na isiyokata tamaa. Simba walinyanyaswa katika eneo la kiungo wakati wa mchezo wa kwanza, na tatizo hilo lilionekana katika michezo yao miwili ya mwisho dhidi ya ligi kuu, dhidi ya Mtibwa na Mgambo. Waliteswa sana na Shaaban Kisiga na Shaaban Nditti wakati wa mchezo wa sare ya bao 1-1 na Mtibwa na wakafunikwa kwa muda mwingi na kiungo Mohammed Samatta wa Mgambo, sasa watakuwa na mtihani wa kujipanga dhidi ya Mazanda.

City si tu kuwa wanajivunia kuwa na timu isiyokata tamaa uwanjani, pia imekuwa chini ya mipango mizuri ya kocha Mwambusi ambaye ameweza kuifanya timu yake kuwa na nidhamu ya mchezo ndani ya uwanja. Tofauti na wachezaji wa Simba, ambao mara zote huishia kucheza kwa viwango vya chini, City wachezaji wao hawachezi kwa kufuata maelekezo ya watu kutoka nje ya bechi la ufundi. Wamepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga, wiki mbili zilizopita, ila waliweza kucheza kwa zaidi ya dakika 40 soka la nguvu ambalo lilifuta pengo la mchezaji wao mmoja aliyeondoshwa uwanjani (Mazanda).

Kama wachezaji wa Simba wataendelea kucheza soka lao kwa kufuata maelekezo ya nje ya benchi la ufundi, watachapwa. Ila kama watacheza kwa nguvu na uvumilivu kwa muda mwingi wa mchezo wanaweza kuwa timu ya kwanza kuvuka ' mwiko na kuifunga' City katika uwanja wake. Sijui kitu gani kilichompa jeuri Rage na kusema kuwa timu itashinda. Alikuwa mbali na timu kwa muda kiasi na mara zote amekuwa akisema kuwa ' Yeye si kocha' anapoulizwa kuhusu matokeo mabaya. Sasa amekuwa kocha? Amechukua nafasi ya Logarusic na kuwaambia wapenzi wa timu yake kuwa watashinda.

 SIMBA IMEIMARIKA...

Walionesha udhaifu mkubwa katika mchezo wa mwezi Oktoba, na kuwaacha City watawale katika mchezo wao wa kwanza ndani ya uwanja wa kisasa, Taifa. Golini kulikuwa dhaifu sana, kipa Abel Dhaira alifungwa mabao marahisi sana, huku lile la mshambuliaji, Nongwa likimfanya watu waanze kuhoji uwezo wake hasa na ubora wake wa kuichezea timu hiyo. Sasa, Dhaira hayupo, na kipa ambaye alionekana kutibu tatizo hilo Ivo Mapunda amekuwa sehemu ya timu hiyo kufungwa na Mgambo alipoutema mpira uliozaa bao pekee, na alifungwa bao la kipuuzi na Mtibwa. Kama ataendelea kupoteza kujiamini kwake bila shaka itakuwa hatari kwa Simba, na ninafikiri ni wakati wa Yaw Berko kucheza mchezo huu kwa kuwa Ivo, yupo katika wasiwasi kwa sasa baada ya timu kupoteza pointi sababu ya makosa yake.

Amis Tambwe alifunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya City, ila ameshindwa kufunga katika michezo dhidi ya Mtibwa na Mgambo huku wengi wakiamini kuwa anakosa msaidizi mzuri katika safu ya mbele ya mashamublizi. Alitengeneza ushirikiano mzuri na Betram Mwombeki na bila shaka mahusiano yao yana faida kubwa kwa timu hiyo. Harouna Chanongo amepoteza kila kitu. Nguvu, hamu ya kuisaidia timu, na amekuwa mchezaji asiye na mchango mkubwa sana katika michezo ya karibuni. Labda pia huu ni wakati wa kocha Logarusic kumuamini kijana William Lucian katika safu ya ulinzi wa kulia, na kumpatia nafasi ya kutosha Mwombeki. Nani mshindi wa mchezo huu?
 
Top