Wamekuwa wakitajwa kuwa washambuliaji hatari ambao umoja wao utaweza angalau kuipeleka United kwenye nafasi za kucheza Champions League msimu ujao.
Robin van Persie na Wayne Rooney wamekuwa wepesi kuelezea namna kila mmoja anavyomkubali mwenzie, na David Moyes ameweka mategemeo yake makubwa kwenye ushirikiano wa washambuliaji wake hao chaguo la kwanza.
Pamoja na imani kubwa waliyonayo mashabiki na benchi la ufundi juu ya ushirikiano huo - ushirikiano wao kwenye dimba unaonyesha hali tofauti.
Katika mchezo wa sare dhidi ya Fulham, Rooney alimpigia Van Persie pasi mbili tu katika mchezo mzima - moja kati ya pasi hizo ilikuwa wakati wa kuanzisha mpira.
Van Persie - ambaye alifunga bao la kusawazisha la United - alimpasi Rooney mara nne tu - kwa mara nyingine tena pasi moja kati hizo nne ilikuwa wakati wa kuanzisha mpira.
Unapofikiria kwamba United walipiga jumla ya pasi 649 katika mchezo huo, ushirikiano baina ya Rooney na Van Persie unatoa tafsiri nyingine - wakiwa hawachangia japo asilimia 1 ya pasi hizo kwa kupasiana wenyewe.
Hivyo inaonyesha ushirikiano wa wachezaji hao wawili unavyoshindwa kufanya kazi. Siku nane zilizopita wakati United walipofungwa na Stoke City wachezaji hao wawili walipigiana jumla ya pasi 6, tatu kati ya hizo zilikuwa wakati wakianzisha mpira.
Mchezo unaofuatia wa United ni jumatano hii wakienda Emirates kupambana na Arsenal, presha ikizidi kumpanda Moyes, timu ikiwa nyuma kwa pointi 9 kutoka kwa timu inayoshika nafasi ya 4. Boss huyo wa United atahitaji washambuliaji wake hao wawe katika kiwango kama ilivyokuwa msimu uliopita ili United angalau iweze kupata matokeo katika huo.
Je Rooney na Van Persie wataweza kuimarisha ushirikiano wao? Majibu yatapatikana Jumatano usiku…..