Cristiano Ronaldo ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Real Madrid tangu ajiunge na miamba hiyo ya soka la Hispania mwaka 2009 akitokea kwa mabingwa watetezi wa ligi kuu soka nchini England, Manchester United.
Wakati akijiunga na Madrid tayari nyota huyo raia wa Ureno alikuwa ni mchezaji bora wa dunia mwaka 2008.
Tangu akiwa Man United, Ronaldo akiwepo uwanjani ilikuwa faida kubwa kwa Sir Alex Ferguson ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa mlezi wa mchezaji huyu.
Na alipotua Real Madrid, amekuwa mchezaji muhimu kwa wakati wote na kila anapokosekana basi imani ya Madrid inashuka.
Wachezaji wenzake na benchi la ufundi wanamheshimu sana Mreno huyo na wanamuona kama mfalme wao.
Ni kweli kila kocha anatamani kuwa na mchezaji kama Ronaldo.
Lakini wapo wachezaji wengine Real Madrid wanaoweza kuamua matokeo wakiwemo Gareth Bale, Angel Dimaria, Karim Benzema na wengineo.
Kwa muda mrefu nyota huyo amekuwa mwamuzi wa matokeo ya Real Madrid, lakini hapo jana mambo yamekwenda taofauti kabisa katika fainali ya kombe la mfalme.
Baada ya kutwaa kombe la Mfalme jana usiku bila Cristiano Ronaldo, kocha wa Real Madrid ameibuka na kusema kukosekana kwa mchezaji huyo kuliwaongezea morali zaidi.
Real iliwatumia Angel Di Maria na Gareth Bale kufunga mabao yake ni kubeba mwari mbele ya FC Barcelona kwenye uwanja wa Mestalla.
Mreno, Ronaldo alikosa mechi ya jana ya `El Clasico`kwa sababu ya kuwa majeruhi.
“Tulistahili ubingwa. Tulicheza kwa umakini na kuwashambulia kwa kushitukiza. Tulicheza vizuri na wachezaji walijituma mno, kwahiyo nawapongeza kwa hilo”.
“Kutokuwepo kwa Ronaldo kuliwapa morali wachezaji. Hali hii iliwafanya wacheze kwa bidii zaidi. Wote walicheza vizuri. Unahitaji kucheza kitimu ili umfunge Barca na tumefanya hivyo”. Amesema Ancelloti.
Madrid wiki ijayo wanatarajia kukutana na Bayern Munich katika nusu fainali ya kwanza ya UEFA, lakini bado wapo katika vita ya kutafuta ubingwa wa La Liga japokuwa Atletico Madrid wanaongoza kwa pointi tatu zaidi na wakibakiwa na mechi tano.
Kwa upande wa Barca, msimu huu wapo hatarini kubaki mikono mitupu baada ya kutolewa UEFA, na jana wamekosa kombe la Mfalme. Pia wiki iliyopita walifungwa na Granada katika mchezo wa La Liga.
Kuhusu Barcelona, Ancelotti amesema;
“Sidhani kama unaweza kuwaondoa kwenye mbio. Wanacheza mpira mzuri japokuwa mambo hayaendi vizuri kwao msimu huu, lakini watapambana mpaka dakika ya mwisho kwenye ubingwa na bado ni wapinzani hatari sana”.
Zaidi Ancelloti ameisifu timu yake kucheza kitimu, lakini anaamini mshindi wa jana ni Gareth Bale.
“Alicheza mpira mzuri mno na kufunga bao muhimu. Lakini wachezaji wote walicheza vizuri”.