WINGA machachari wa Chelsea, Eden Hazard yuko hatarini kukosa mechi ya kwanza ya nusu fainali ya UEFA dhidi ya Atletico Madrid kutokana na kusumbuliwa na majeruhi.
Hazard alitolewa katika mchezo wa robo fainali dhidi ya PSG ambapo walishinda mabao 2-0 na kufuzu nusu fainali kwa wastani wa mabao 3-3, lakini Chelsea walikuwa na faida ya bao la ugenini.
Kocha msaidizi wa Chelsea Steve Holland mapema wiki hii alisema Hazard anaendelea vizuri na anaweza kucheza, lakini taarifa za leo ijumaa ni mbaya zaidi kwasababu nyota huyo hatakuwa fiti kwa mechi hiyo.
“Sio kwamba Hazard hataweza kuimarika, lakini kushindwa kufanya mazoezi na timu inaashiria wasiwasi kwa yeye kucheza”. Alisema taarifa ya Holland kwa waandishi wa habari.
Kabla ya kwenda kucheza nusu fainali ya UEFA katika uwanja wa Vicente Calderon, Chelsea watasafiri kuwafuata vibonde wa ligi kuu soka nchini England, klabu ya Sunderland, mechi inayoaminika kuweka wazi kama Mourinho ataendelea kuwepo katika mbio za ubingwa.
Katikati ya wiki, mashabiki wa soka walishuhudia Sunderland wakiwakazia Manchester City na kutoka sare ya 2-2, lakini kama Chelsea watashinda mechi hiyo na nyingine zote zilizobaki wanaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kubeba mwari.
Holland aliendelea kwa kusema: “nafasi ya kwanza, pili na tatu inawezekana kwa timu zote tatu za juu. Timu zinakaribiana sana kwa pointi. Lakini ndio timu iliyocheza mechi nyingi zaidi msimu huu”.
“Ni msimu wenye changamoto kubwa, hakika unaumiza kichwa sana. Nadhani uzoefu ni muhimu katika mashindano yoyote yale. Tunao wacheza wenye uzoefu kwenye kikosi, nadhani watatusaidia”.
“Mechi ya kesho ni muhimu mno kwetu. Siamini kama ubingwa wa msimu huu utaamuriwa katika mechi yetu na Liverpool. Mchezo wa kesho na Sunderland ni mgumu zaidi na tunahitaji kuingia kwa umakini mkubwa”