212238hp2Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU ya Taifa ya Kenya, `Harambee stars` imelazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Comoros katika mchezo wa marudiano wa kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Harambee Stars waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza mjini Nairobi na sare ya leo inawafanya wasonge mbele kwa wastani wa mabao 2-1.
Hata hivyo katika mchezo wa leo, Kenya ilimkosa mchezaji wake wa kimataifa, Denis Oliech ambaye aliondolewa kikosini kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Rais wa shirikisho la soka Kenya, KFF, Sam Nyamweya amesema wamepambana kwa nguvu zote kuhakikisa kuwa wanapata matokeo.
Nyamweya aliongeza kuwa Comoros walijidhatiti katika mchezo wa leo, lakini wanashukuru vijana wao wamejituma na kusonga mbele.
Kuelekea katika mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe keshokutwa jumapili, Nyamweya ameitakia kila la heri timu ya taifa ya Tanzania.
Rais huyo alisema Tanzania ni majirani wazuri wa Kenya, hivyo watafurahi kuona Taifa stars inasonga mbele kama wao.
Mechi nyingine inayopigwa leo ni baina ya Sudan Kusini dhidi ya Msumbiji.
Mechi ya kwanza iliyopigwa mjini Maputo, Msumbiji waliibuka na ushindi wa mabao matano.
Msumbiji wanahitaji kutofungwa mabao zaidi ya matano ili kusonga mbele, na wakishinda watakutana na mshindi wa jumla baina ya Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe.

 
Top