ndumbalo1
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAGOMBEA wawili , Evans Eliez Aveva na Andrew Peter Tupa wamepitishwa kugombea Urais wa klabu ya Simba katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu, jijini Dar es salaam.
Akizungumza leo mchana na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa shirikisho la soka la Tanzania, TFF, mtaa wa Ohio, Posta, jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Wakili Dkt. Damas Daniel Ndumbaro alisema wagombea wote waliopitishwa ni sasa ruksa kuanza kampeni.
Hata hivyo kampeni hizo lazima ziwe za ustaarabu, heshima na kutotumia lugha ya matusi.
Aidha, Wakili Ndumbaro aliwataja wagombea wanne katika nafasi ya umakamu wa Rais ambao ni Geofrey Nyange Kaburu, Jamhuri Musa Kiwhelo `Julio`, Bundala Kabulwa na Swedi Nkwabi. 
Nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji upande wa wanaume watu 18 wamevuka kigingi ambao ni Yasini Mwete, Ally Suru, Said Tully, Rodney Chiduo, Said Pamba, Ally Chaurembo, Abdulhamid Mshangama, Chano Almasi, Damian Manembe, Ibrahim Masoud, Kajuna Noor, Hamisi Mkoma, Alfred Elia, Saidi Kubenea, Idd Mkamballah, Juma Mussa, Maulid Abdallah na Collin Frisch.
Kwa upande wa wanawake wamepitishwa watu watatu ambao ni Asha Muhaji, Jasmine Badour na Amina Poyo.
Uchaguzi wa Simba kwa muda mrefu umegubikwa na mizengwe iliyotokana na kuenguliwa kwa jina la mgombea wa Urais, Michael Richard Wambura.
Baada ya kuenguliwa, Wambura alikata Rufaa katika kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya akipinga kuenguliwa kwa jina lake na baadaye alishinda.
Lakini aliondoshwa kwa mara ya pili kwa kupiga kampeni kabla ya muda.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa baadhi ya wanachama wanamuunga mkono Wambura wameshatua mahakani wakitaka mahakama isimamishe uchaguzi uliopangwa kufanyika juni 29.
Wanachama hao wanaosemekana kuwa wafuasi wa Wambura wanadai kamati ya uchaguzi na kamati ya rufani ya TFF haikumtendea haki Wambura, hivyo wanaiomba mahakama isimamishe uchaguzi huo.

 
Top