DSC07132
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MICHAEL Richard Wambura ameibuka tena na kumshangaa Rais mpya wa Simba,  Evans Elieza Aveva na kamati yake ya utendaji kwa kufanya maamuzi ya kulipeleka suala lake kwenye mkutano mkuu wa agosti 3 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Wambura amesema hakuna haja ya kupeleka suala lake kwenye mkutano huo kwasababu sakata lake lilimalizwa na kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wake,  Jaji Julius Mutabazi Lugaziya.
Wambura ameyasema hayo ikiwa ni jana tu,  ambapo Aveva alitangaza kuwasimamishwa wanacha 69 kwa kosa la kwenda mahakama ya kawaida kujaribu kuzuia uchaguzi wa Simba na alisema suala lao litajadiliwa kwenye mkutano mkuu wa mwezi agosti, sanjari na suala la Wambura la kuipeleka Simba mahakamani mwaka 2010.
Lakini `Kidume` Wambura amekuja juu na kusema yeye alishasafishwa na kamati ya Lugaziya na kitendo cha Aveva kuwapiga `Stop` wanachama ni kuendelea kuchochea migogoro isiyokuwa ya lazima.
“Mimi nilisafishwa kwenye kamati  ya Rufani ya Lugaziya na ndio maana nilirudishwa kwenye mchakato wa uchaguzi, na niliondolewa kwa kosa la kupiga kampeni kabla ya muda, hivyo sina haja na mkutano huo”. Alisema Wambura.
Wambura aligusia Ibara ya 41(d) ya klabu ya Simba ambapo alifafanua kuwa kuwanyima wanachama fursa ya kujitetea na kusikilizwa kabla ya kuchukua hatua ni uvunjifu wa haki za msingi za binadamu.
Aidha,  Wambura alisema wanachama waliokwenda mahakamani wasipuuzwe kwasababu wana hoja za msingi.
“Wangekuwa hawana hoja, hata mahakama kuu isingewapa haki ya kufungua shauri lao. Wasipuuzwe, wapewe fursa ya kujitetea na kusikilizwa”. Aliongeza Wambura.
Alisisitiza kuwa Ibara ya 54(3) ya klabu ya Simba inafafanua kuwa uamuzi wowote wa kufukuza wanachama lazima upigiwe kura za siri na wajumbe theluthi mbili waunge mkono, huku akitolea mfano wa Hassani Dalali alipofanya jaribio la kumpinuda Mwina Kaduguda, lakini alikwama kwasababu wanachama walikataa pendekezo lake.
Aliongeza kuwa uongozi wa Aveva hauwezi kupambana na wanachama zaidi ya 500 na kama utaendelea kufanya hivyo basi utaingia katika mgogoro mkubwa, lakini akashauri uongozi utafute suluhusho la mapema.
Wambura alisema ushauri wake atauwasilisha kwa maandishi kwa uongozi wa Simba sc kama sehemu kutunza kumbukumbu kuwa aliyaongea hayo.

 
Top