Mbrazil, Jaja hakufanikiwa kugusa nyavu katika mechi ya pili ya ligi kuu
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
LIGI kuu soka Tanzania bara imeendelea leo kwa viwanja viwili kuwaka moto jijini Dar es salaam.
Yanga wakicheza uwanja wa Taifa wamefanikiwa kuitungua 2-1 Tanzania Prisons maarufu kwa jiana la ‘Wajelajela’
Mabao ya Yanga yalifungwa na Andrey Coutinho katika dakika ya 34 na Saimon Msuva dakika ya 69, wakati bao la kufutia machozi la Prisons lilitiwa kimiani na Ibrahim Isaka Hassan.
Mechi nyingine imepigwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam baina ya wenyeji JKT Ruvu dhidi ya Kagera Sugar.
Mabao mawili ya Rashid Mandawa na Salum Kanon yalitosha kuipa Kagera Sugar ushindi wa 2-0 dhidi ya maafande hao wanaonolewa na kocha mkongwe, Fred Felix Minziro.
Licha ya kuibuka na ushindi, Kagera walitawala mchezo huo kwa kiasa kikubwa na kuwanyima nafasi JKT Ruvu walioonekana kukosa mipango leo.
Vijana wa Minziro walishindwa kufurukuta na kukosa nidhamu ya mchezo na kujikuta wakifanya makosa mengi. Hata nafasi chache walizopata walishindwa kuzitumia.
Kagera Sugar kwa jinsi ilivyocheza leo, si timu ya kuidharau. Imekaa poa kwa kiasi kubwa, hivyo inaweza kutoa changamoto nzuri.
Ligi hiyo itaendelea wikiendi ijayo (Oktoba 4 na 5 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka uwanjani.
Oktoba 4, Polisi Morogoro watakuwa nyumbani uwanja wa Jamhuri kuikaribisha Kagera Sugar.
Coastal Union wakakuwa nyumbani CCM Mkwakwani Tanga kuchuana na Ndanda fc.
Simba wataikaribisha Stand United katika mechi ya tatu ndani ya dimba la nyumbani la Taifa jijini Dar es salaam.
Mechi nyingine itawakutanisha Tanzania Prisons dhidi ya Azam fc katika uwanja wa Sokoine Mbeya.
Ruvu Shootings itaialika Mbeya City fc katika uwanja wake wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Oktoba 5 mwaka huu, Yanga watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa kukabiliana na JKT Ruvu.
Mechi ya mwisho itakuwa baina ya Mtibwa Sugar na Mgambo JKT katika uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.
Baada ya mechi hizo, ligi itasimama kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Taifa Stars dhidi ya Benin itakayopigwa Oktoba 12 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Kivumbi cha ligi kuu kitaendelea Oktoba 18 ambapo mechi kubwa itakuwa baina ya Yanga na Simba sc uwanja wa taifa .