Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
RAUNDI ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea wikiendi hii kwa timu zote 14 kushuka dimbani.
Kesho jumamosi (septemba 27 mwaka huu), Wekundu wa Msimbazi, Simba sc wenye kumbukumbu ya kutoka sare ya 2-2 na Coastal Unioni wikiendi iliyopita watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa, Dar es salaam kuchuana na Polisi Morogoro.
Katika mechi ya ufunguzi, septemba 20, Polisi Moro walifungwa mabao 3-1 na Mabingwa watetezi, Azam fc.
Mtibwa Sugar wenye kumbukumbu ya kuifunga Yanga 2-0 katika mechi ya ufunguzi uwanja wa Jamhuri wikiendi iliyopita wataikaribisha Ndanda fc ya Mtwara iliyoshinda 4-1 dhidi ya Stand United katika mechi ya ufunguzi uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Azam fc walioshinda 3-1 mechi iliyopita wataikaribisha Ruvu Shootings iliyofungwa 2-0 katika mechi ya ufunguzi uwanja wa Mabatini, Pwani.
Mbeya City fc iliyotoka 0-0 na JKT Ruvu itakuwa uwanja wa nyumbani wa Sokoine kwa mara nyingine kuwakaribisha Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga.
Coastal wao walitoka sare ya 2-2 na Simba katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa wikiendi iliyopita uwanja wa Taifa.
Mgambo JKT walioshinda 1-0 mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar watakuwa nyumbani CCM Mkwakwani Tanga kuchuana na Stand United waliotandikwa 4-1 na Ndanda fc katika mechi ya ufunguzi, uwanja wa Kambarage.
Ligi hiyo itaendelea jumapili (septemba 28) ambapo mechi mbili zitapigwa.
Yanga wenye kumbukumbu ya kupigwa 2-0 mechi iliyopita uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa, Dar es salaam kuwakaribisha Prisons walioshinda 2-0 mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting.
JKT Ruvu waliotoka 0-0 na Mbeya City fc Sokoine Mbeya, watakuwa nyumbani Azam Complex kuchuana na Kagera Sugar waliotandikwa 1-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Mgambo JKT.