Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
YANGA kuifunga Simba katika mechi ya kirafiki, bonanza au mashindano ni faida kubwa kwa kocha na wasaidizi wake, vivyo hivyo kwa upande wa pili.
Makocha wengi wa nyuma waliwahi kusifiwa na kuonekana bora kwa kitendo cha kumuadhibu mtani wa jadi, na wale waliozichomesha timu zao mbele ya mtani walitimuliwa kirahisi tu.
Hata wachezaji wanaofanya vizuri baina ya watani wa jadi wanaonekana moto wa kuotea mbali kuliko wale wanaofanya vizuri kwenye mechi dhidi ya timu nyingine.
Sahizi Simba na Yanga zipo chimbo kujiandaa na ligi kuu msimu wa 2014/2015 unaotarajia kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Yanga wataanza kampeni zao septemba 20 mwaka huu uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati siku inayofuata (septemba 21) Simba watakuwa uwanja wa Taifa kuivaa Coastal Union.
Mashabiki na viongozi wa timu hizi mbili wanatambiana vikali mno kila mmoja akisema mtani atakiona cha moto.
Wanajangwani wanakwambia ‘Okwi mwisho Chalinze, kila mtu mjini Jaja’. Wanamsimbazi nao wanatamba na urejeo wa Okwi wakisema kipigo cha 5-0 kipo njiani.
Andrey Coutinho wa Yanga naye anatumika na wanayanga kuichimba Mkwara Simba, huku nako kuna mtu anaitwa Paul Kiongera.
Juzi uwanja wa Taifa,Dar es salaa, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ alifunga mabao mawili katika ushindi wa Yanga wa 3-0 dhidi ya Azam fc mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kupenuliwa kwa pazia la ligi kuu.
Baada ya kitendo hicho, Jaja aliteka jiji zima, kila kona Jaja tu. Na wanayanga waliimba nyimbo na kumsifia sana Mbrazil huyo licha ya siku za karibuni kuona hana uwezo.
Sasa wimbo ni Oktoba 12 mwaka huu ambapo timu hizo zitakutana. Mashabiki wa Yanga wanatamba kuwa Jaja atawamaliza Simba, nao wa Msimbazi wanatamba na nyota wao Pual Kiongera aliyefungwa mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0, mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia, uwanja wa Taifa, septemba 6 mwaka huu.
Mbali na Kiongera, Simba wanajivunia mfungaji bora wa msimu uliopita, Mrundi, Amissi Tambwe.
Binafsi sioni kama tambo hizi zina maana yoyote katika maendeleo ya mpira wa miguu wa nchi hii. Nadhani imechangiwa na mitazamo mifupi ya mashabiki wengi wa soka na viongozi kwa ujumla.
Leo hii unamsikia kiongozi wa juu wa Yanga au Simba akizungumzia namna wanavyojiandaa kumfunga mpinzani mabao 5-0 au 8-0.
Utani wa jadi ni muhimu katika soka, lakini wenzetu wa ulaya wanakuwa na mipango ya mashindano makubwa zaidi ya ligi kuu.
Mashabiki wa Manchester United wanapenda sana kuona timu yao inawafunga mahasimu wao Manchester City, ua Barcelona kwa Real Madrid, lakini wakati huo huo wanapenda kuona timu zao zinafanikiwa UEFA.
Wenzetu wanathamini sana michuano kama UEFA na huwa wanawekeza fedha na muda kujiandaa nayo. Ndio maana ukiwasikia makocha wengi au viongozi, huwa wanasema msimu huu utakuwa mgumu kwetu kwasababu tunakabiliwa na UEFA.
Kama timu haichezi UEFA kama ilivyokuwa kwa Liverpool msimu uliopita au Manchester United kwa msimu huu inapewa nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
Hapa unagundua kitu kimoja muhimu kuwa licha ya Chelsea kumsajili Diego Costa ili aifunge Arsenal, Man United na timu nyinginezo, lakini wanawaza zaidi kuzifunga timu nyingine za ulaya katika michuano ya UEFA.
Kwahiyo wenzetu wanajua fika kuwa kuna maana kubwa kutwaa taji la UEFA kuliko ligi kuu, ingawa ni muhimu zaidi kutwaa kombe la ligi kuu au kushika nafasi nzuri ili ushiriki UEFA.
Sisemi ligi kuu sio muhimu, kuna ulazima wa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kucheza michuano mikubwa.
Simba hawana michuano ya kimataifa mwakani. Nguvu zote zinaelekezwa katika michuano hiyo ili kutwaa kombe na kupata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa au kombe la shirikisho mwakani endapo watashika nafasi ya pili.
Ni halali kwa Simba kuifikiria ligi kuu, lakini sio kuifikiria Yanga tu. Kwasababu hawawezi kushinda kombe kwa kumfunga Mtani pekee.
Yanga asiwe kichwani mwao muda wote, wafikirie kuwa kuna Azam fc, Mbeya City fc, Kagera Sugar, Ruvu Shootingm Mtibwa Sugar na nyinginezo.
Nadhani ule wakati wa kuweka mikakati ya mechi ya mtani, kuificha timu na kwenda kwa wataalamu wa mambo yale ya kutambika, umepitwa na wakati. Inatakiwa timu kuandaliwa kwa mechi zote 26.
Sidhani kama fikira za Patrick Phiri ziko sawasawa na mashabiki wake wanaofikiria namna Okwi atakavyoifunga Yanga.
Jaja kwa sasa ndio wimbo wa mjini
Malengo ya Phiri ni kushinda mechi zote kwasababu itazidi kujenga wasifu wake hata akiondoka Tanzania. Huwezi kuajiriwa kwa CV ya kumfunga Mtani, hapana! .
Kwa upande wa Yanga wakumbuke kuwa wana majukumu mazito kuliko Simba. Watashiriki kombe la shirikisho na ligi kuu.
Nategemea kuona wanayanga wakitamba kuwa tumemsajili Jaja, Al Ahly tukikutana nao watatukoma. Wanatakiwa kufikiria mbali zaidi na kujenga heshima.
Mawazo ya kuifikiria Simba wakati utacheza kombe la shirikisho, ni kukosa maono kabisa. Imefika wakati timu zetu zitakazowakilisha nchi zifikirie mambo mawili kwa uzito wa juu. Yaani Yanga wawaze Kombe la shirikisho na ligi kuu.
Emmanuel Okwi (kushoto)
Waiandae timu kwa misingi hiyo na sio kuifikiria Simba. Kama watafungwa na Simba, lakini wakafanya vizuri kombe la shirikisho, kutakuwa na faida kubwa kimpira kuliko kuifunga Simba, halafu wanatolewa raundi ya awali.
Leo hii kiongozi anaonekana wa maana kwasababu amemfunga mtani. Tena hawana aibu kusema naangia madarakani kuwakomesha mahasimu wetu.
Yaani unapigiwa kura eti ukamfunge mtann? Tuna malengo ya kulisongesha soka letu?
Nakuwa na furaha sana ninapomsikia kiongozi akisema tunaiandaa timu kwa michuano ya kimataifa, tunataka kuifikisha timu anga za kimataifa, lakini nakereka sana ninaposikia mtu anasema tunaiandaa timu, msimu huu Simba na Yanga hawatoki.
Mwisho wa siku wanazikamia mechi na kutoa sare, lakini wakikutana na timu nyingene, wanachemsha. Wengine wanashuka daraja, wengine wanashika nafasi za mkiani.
Kwa mfano Azam fc mwakani wanashiriki ligi ya mabingwa. Haina maana kuingia katika siasa za kuifunga Simba au Yanga.
Wao wanatakiwa kufikiria timu pinzani za ligi ya mabingwa, lakini kwa vile viongozi wamekosa maono, wanakesha kufikiria kuzifunga Simba na Yanga.
Hatuwezi kuendelea kwa kushindana wenyewe. Unataka Jaja aifunge Simba au Kiongera aifunge Yanga na si TP Mazembe?
Lazima tuachane na mambo ya kizamani. Kocha asifukuzwe kwasababu amefungwa na mtani. Ni kitu cha kawaida, mbona Man United hata kama watafungwa nje-ndani na Man City wanawaacha makocha?
Vipi kwa Real Madrid inapofungwa na Barcelona, nje-ndani, makocha wanatimuliwa?, hapana! Wanaangalia michezo yote ya ligi. Kama timu haijafanya vizuri, wanachukua maamuzi.
Najua Maximo anawaza mbali kuliko mashabiki na viongozi wanaowaza kuifunga Simba. Naamini Phiri anawaza mbali zaidi ya kuifunga Yanga.
Kufundisha mpira ni kazi yao. Anaweza kuajiriwa popote pale, na ndio maana wanajitahidi kushinda makombe ili kujenga wasifu utakaowasaidia mbeleni.
Mashabiki badala ya kuwasaidia kwa mipango mizuri, tunafurahia wamfunge mtani tu, biashara imekwisha, tutafika?
Siku njema!