hans-poppe
Ameshinda? : Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KAMA ubongo wako una uwezo mzuri wa kutunza kumbukumbu, Ijumaa ya Agosti 29 mwaka huu klabu ya Young Africans ilitangaza kumshitaki mchezaji Emmanuel Okwi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuwasilisha nakala kwa shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) na shirikisho la soka duniani (FIFA) kwa kuingia mkataba na timu nyingine wakati akiwa bado ana mkataba wa miaka miwili. Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji aliwaambia waandishi wa habari siku hiyo kuwa uongozi wa klabu huyo ulishangazwa na kitendo cha viongozi Simba , wakala na mchezaji mwenyewe kuingia mkataba wa miezi sita kwa madai kuwa anataka kulinda kiwango chake wakati akiwa na kesi na Yanga. Manji alisema awali Yanga walipeleka malalamiko TFF na kuwapa nakala CAF na FIFA kuwa Emmanuel Okwi awali alifanya mazungumzo na timu ya Wadi Degla FC ya nchini Misri na kufikia klabu hiyo kutuma ofa ya kutaka kumnunua bila kuwasiliana na uongozi wetu. Wakati Yanga wakisubiri majibu kutoka TFF wakashangaa kuona mchezaji huyo amesaini mkataba mwingine, na wakadai mchezaji huyu alikuwa akirubuniwa na watu na kufikia hatua ya kusaini mkataba mwingine kitu ambacho alikiuka sheria za FIFA za usajili. Baada ya kuona amesaini mkataba na Simba, Yanga walichokifanya ni kuandika barua nyingine TFF juu ya suala hilo na kuomba kulipwa fidia ya US Dollar 500,000 (sawa na TZS 800,000,000/=) kutoka kwa klabu ya Simba, wakala wake na mchezaji mwenyewe.
Amechemsha?: Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji (kulia) siku alipotangaza kumshitaka Okwi. Kushoto ni makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga.
Aidha uongozi wa Yanga uliomba TFF kulipatia ufumbuzi suala hilo ndani ya siku saba, na kama siku saba zikikipita basi uongozi wa Jangwani utakwenda moja kwa moja FIFA na ikishindakana mahakama ya soka CAS, lakini hilo halikufanyika hata kama TFF hawakutelekeza ndani ya siku hizo saba. Yanga waliongeza kuwa lengo lao halikuwa kuikomoa timu ya Simba, bali walichotaka ni sheria ifuatwe, kwani Okwi alikua ameitumikia klabu ya Yanga kwa kipindi cha miezi sita tu, na kuwa amebakiza mkataba wa miaka miwili mpaka mwishoni mwa 2015/2016.
Sheria iko wazi kabisa mchezaji anayekutwa na kosa la kusaini sehemu mbili adhabu yake ni kufungiwa kucheza soka kuanzia mwaka mmoja na kuendelea huku klabu husika ikifungiwa kusajili kuanzia miaka mwili na kuendela na kushushwa daraja au adhabu zote kwa pamoja. Jana (septemba 7 mwaka huu), kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la soka Tanzania TFF ilikutana kujadili mgogoro huo wa kimkataba baina ya Okwi na klabu yake ya Yanga. Kamati ilisema kilichokuwa kikijadiliwa sio usajili wa Okwi bali ni suala la kimkataba.Kwa maana hiyo, Simba haikujadiliwa hata kidogo, bali ni Okwi na Yanga. Katika kikao cha jana, mkataba huo ulipitiwa vizuri, mchezaji akasikilizwa na upande wa Yanga nao wakapewa nafasi, lakini mwisho wa siku ikabainika kuwa mkataba baina ya pande hizo mbili umevunjika, kwa mujibu wa kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji. Kwanini umevunjika? Jibu likawa rahisi sana. Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga akiwa mwajiri, alikiuka kipengele cha 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili. Yanga haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba uvunjwe. Kutokana na hilo, Okwi ni mchezaji huru na anaruhusiwa kujiunga na klabu yoyote ikiwemo Simba ambapo amesaini mkataba wa miezi sita. Stori ya Okwi iliteka hisia za mashabiki wengi wa mpira wa miguu nchini kwasababu ilihusisha klabu mbili kongwe, Simba na Yanga.
Mkali wa sheira?: Emmanuel Okwi (kulia) akiwaonesha ufundi wachezaji wa Gor Mahia siku ya jumamosi uwanja wa Taifa, Simba ikishinda 3-0
Mara kadhaa klabu hizi zinapigana vikumbo katika usajili na kama una kumbuka usajili wa Mbuyu Twite Jr ulizifanya klabu hizi zivutane vikali, lakini mwisho wa siku Yanga wakaibuka videdea. Safari hii Simba hakuwa na tatizo lolote na Yanga kwa mujibu wa maelezo ya hapo, lakini Okwi alikuwa na tatizo na Yanga. Kutokana na upinzani mkubwa wa klabu hizi kongwe, Simba nao walikuwa wakizungumzwa mtaani kama wameifanyia kitu mbaya Yanga juu ya mchezaji huyo. Kumbe kisheria haikuwa hivyo. Okwi na Yanga ndio walikuwa wanapambana. Pia kulikuwa na pingamizi la Coastal Union juu ya usajili wa Abdi Banda kujiunga na Simba. Coastla walidai bado wana mkataba wa miaka miwili na Banda na walitangaza kumfungia mwaka mmoja kucheza soka kwa kitendo cha kusaini mikataba miwili. Kumbe Coastal nao walikiuka kipengele cha kimkataba ambapo walishindwa kumlipa mchezaji mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba linavyotaka. Coastal Union iliwakilishwa na kiongozi mmoja wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake. Tofauti ya Okwi na Banda ni ndogo tu, lakini kwa asilimia kubwa sakata lao linafanana. Yanga walishindwa kutimiza malipo ya ada ya usajili kama takwa la kimkataba, wakati Coastal walishindwa kumlipa mchezaji mshahara kama takwa la mkataba linavyosema. Ukiangalia masakata haya mawili, kuna watu walishindwa kutimiza majukumu yao kwa upande wa Yanga na Coastal Union.
Wametengana: Emmanuel Okwi (kulia) alicheza na Mganda mwenzake, Hamis Friday Kiiza wakiwa Yanga sc msimu uliopita.
Mkataba ni suala la kuheshimika. Kila kipengele kina maana kubwa na kushindwa kutekeleza kimoja tu au sehemu ndogo ya mkataba unaweza kupoteza haki yako. Yanga kwa kushindwa kutekeleza kipengele cha 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili wamepoteza haki ya kummiliki Okwi aliyebakiza miaka miwili katika mkataba wake, hali kadhalika Coastal Union kwa Banda. Kuna picha inanijia kichwani mwangu kuwa klabu kubwa za hapa nchini hazina mfumo mzuri wa kusimamia mikataba yao na hata uvunjwaji wa mikataba ya wachezaji unakuwa na mapungu mengi.Hii pia inachangiwa na ueledi mdogo wa wachezaji wa soka la Bongo katika masuala ya mikataba. Leo hii ukiuliza ni wachezaji wangapi wana wanasheria wao?Jibu ni wachache tu. Na ndio maana viongozi wa Yanga na Simba na klabu nyingine wanakuwa na jeuri ya kujivunjia mikataba na hawalipi haki za wachezaji. Kuna lundo kubwa la wachezaji wamevunjiwa mikataba bila kulipwa haki, lakini kwakuwa wengi ni “mambumbu’ wamekaa na kulia kilio cha samaki. Samahani kwa neno hili, lakini inabidi nilitumie tu. Unakumbuka sakata la John Njoroge, Wisdom Ndlovu na Yanga au kocha Papic na Yanga? Ilikuwa ni madhara ya kuvunja mkataba kiholela. Hata Simba nao walishawahi kuingia kwenye matatizo ya kuvunja mikaba na wachezaji bila kuwalipa haki zao. Lipo kundi kubwa la wachezaji hao, lakini sitalitaja kwa leo. Ukiangalia suala la Okwi, sio gumu kabisa. Mganda huyu ana akili nyingi na anazifahamu vizuri sheria za kimkataba. Hata kama sio yeye binfasi, basi nyuma ana washauri wazuri wa kisheria. Anapoamua kitu ujue anajua kwa kutokea. Unakumbuka sakata la Okwi na Etoile Du Sahel ya Tunisia?
 Kashinda kesi: Abdi Banda naye ruksa kucheza Simba sc
Simba ilimuuza Okwi kwenda klabu hii kwa zaidi ya shilingi milioni 400, lakini kitendo cha Etoile kukiuka kipengele kimoja cha mkataba, nyota huyu aliwamaliza. Timu hii haikumlipa mshahara kwa miezi mitatu kama takwa la kimkataba, lakini iliwahi kuelezwa kuwa Etoile walifanya hivyo kama sehemu ya adhabu kwa Okwi kwani alikaa muda mrefu bila kurudi kambini baada ya kuruhusiwa kuichezea timu ya Taifa ya Uganda. Okwi alipeleka kesi FIFA akipambana na Etoile. Simba nao walikuwa wanapambana na Etoile ili walipwa fedhe zao za usajili. FIFA baada ya kuona Okwi amekaa muda mrefu bila kucheza, walimpa ruhusa ya kucheza kwa muda wa miezi sita katika Sport Club Villa ya Uganda ili kulinda kiwango chake wakati kesi yake inasubiriwa. Villa walimuuza Okwi kwenda klabu ya Yanga na mengi yakaibuka juu ya suala hilo. Kumbe Okwi alikuwa na haki kwasababu hakutekelezewa kipengele cha mkataba na akawa mchezaji huru na ndio maana majogoo wa Kampala walimuuza.
Mkali wa Msimbazi, Okwi (kushoto)
Suala hili linafanana na la Abdi Banda kwa kiasi Fulani. Coastal wanadai kinda huyu alikataa kuchukua mshahara baada ya kurubuniwa na watu, lakini kiukweli ni nani atakwepa kuchukua mshahara wake? Baadaye mkataba ukavunjika kwa kushindwa kumlipa mshahara wa miezi mitatu mfululizo na akawa mchezaji huru. Ukifuatilia sakata la Okwi na Banda, Simba haikuwa na tatizo na Yanga wala Coastal Union, bali wachezaji walikuwa na matatizo na tmu zao. Kwa namna Simba walivyoweza kutafsiri sheria za kimkataba za wachezaji hawa na kuona ni sahihi kuwasajili, nadhani mwenyekiti wa kamati ya Usajili YA Simba, Zacharia Hans Poppe amewapiga bao wapinzani. Alijiamini wakati wa usajili huu kwasababu wanasheria waliweza kumtafsiria vizuri mikataba ya wachezaji hawa na kuona imevunjika kisheria. Kwa hapa Hans Poppe amefanikiwa kuwa makini na hatimaye ameibuka mshindi. Lakini kwa viongozi wa Yanga na Coastal Union wamechemsha kwa hili. Najua sio wao tu, wapo wengine wenye ueledi mdogo juu masuala ya kisheria. Hata kama Yanga watakwenda CAF au FIFA au mahakama ya Rufani ya juu ya michezo, sidhani kama itakuwa rahisi kushinda kama walikiuka kipengele cha 8 cha mkataba. FIFA watakuwa na majibu yale yale kama ya kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji. Rejea Okwi na Etoile Du Sahel. Labda suala la kuongea na klabu ya Misri na kufikia makubiliano bila ruhusa ya Yanga linaweza kuwa la msingi kwa sasa. Hapa kuna hoja ya Msingi kama kweli jambo hili lilitokea. Ni marufuka kuongea na mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine bila ruhusu ya timu inayommiliki. Viongozi wa mpira wa miguu nchini, jifunzeni kuheshimu vipengele vya mikataba ya wachezaji. Jumatatu njema!

 
Top