MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara imekamilika
Jumapili ambapo jumla ya mabao 18 yamefungwa ikiwa ni michezo ya kwanza
kwa timu zote 14 zinazo shiriki Ligi hiyo.
Mechi hizo za kwanza zimeonyesha maajabu makubwa ambayo huenda
yakazidi kushangaza wadau wa soka msimu huu kwa timu ngeni katika ligi
hiyo Ndanda FC,kutoka Mtwara kuongoza ligi baada ya kuwafunga wageni
wenzao Stend United mabao 4-1,huku bingwa Mtetezi Azam ikishinda mabao
3-1
Simba na Yanga zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri
kwenye mechi zao za awali mambo yalikuwa magumu kwao baada ya kujikuta
zikikabwa koo Yanga iliyokuwa ugenini Jamuhuri Morogoro ilifungwa mabao
2-0 na Mtibwa Sugar na Simba ikatoka sare ya 2-2 na Coastal Union siku
iliyofuata Jumapili.
Mbeya City ambayo ilikuwa tishio katika ligi hiyo nayo mambo hayakywa
mazuri Jumamosi baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na
Maafande wa JKT Ruvu inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga Fredy
Felix Minziro wakati siku hiyo Mgambo JKT ikatoa kipigo cha bao 1-0 kwa
Kagera Sugar kwenye uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Ruvu Shooting, ya Pwani nayo ilianza ligi hiyo vibaya msimu huu baada
ya kufungwa nyumbani mabao 2-0 na Tanzania Prisons,matokeo ambayo
yamemuumiza mno kocha wake Mkenya Tom Olaba kutokana na maandalizi
ambayo wameyafanya kuelekea msimu huu.
Lakini matokeo hayo kwa kifupi yanaonyesha uhalisia wa ligi ya msimu
huu wa 2014/2015, itakavyokuwa ngumu na yenye ushindani kutokana na timu
nyingi kufanya maandalizi mazuri tofauti na ilivyokuwa misimu
iliyopita.
Misimu iliyopita ilikuwa vigumu kuona timu ikipata ushindi ugenini
lakini katika mechi za kwanza msimu uliopita katika mechi saba zilizo
chezwa siku ya ufunguzi Jumamosi timu mbili za Ndanda Fc na Tanzania
Prisons zilipata ushindi ugenini huku JKT Ruvu na Coastal Union
iliyocheza na Simba Jumapili kwenye uwanja wa taifa zikipata sare
ugenini.
Hii inaonyesha namna ambavyo soka la Tanzania linavyo piga hatua kwa
kasi kadiri siku zinavyokwenda lkwa sababu misimu iliyopita ilikuwa siyo
rahisi kuona Yanga au Simba zikipoteza mechi za awali kama ilivyotokea
msimu huu.
Raundi ya pili itaendelea Jumamosi hii ambapo Simba itaendelea kubaki
Dar es Salaam kwenye uwanja wa taifa kuwakabili Polisi Moro, ambayo
ilifungwa mabao 3-1 na Azam katika mechi ya ufunguzi,Vinara Ndanda
FC,bado watakuwa ugenini Morogoro kucheza na wababe wa Yanga Mtibwa
Sugar na Azam siku hiyo itacheza na Ruvu Shooting kwenye uwanja wake wa
Azam Complex Chamazi.
Mbeya City nao wataendelea kubaki nyumbani uwanja wa Sokoine Mbeya
kuialika Coastal Union na mchezo wa mwisho siku hiyo utapigwa kwenye
uwanja wa Mkwakwani Tanga wakati wenyeji Mgambo JKT watakapoikaribisha
Stend United kutoka Mkoani Shinyanga.
Jumapili kutakuwa na mechi mbili zote zikifanyika mkoa wa Dar es
Salaam Yanga iliyofungwa mabao 2-0 na Mtibwa itakuwa uwanja wa nyumbani
wa taifa kuwaalika Tanzania Prisons na JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa
Kagera Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex.