Loic Remy, alipigwa picha akifanya mazoezi kujiandaa na mechi ya Chelsea dhidi ya Swansea leo jumamosi
JOSE Mourinho akijiandaa kumtambulisja Loic Remy ameanika hadharani kuwa anajivunia sana usajili wa Chelsea majira ya kiangazi mwaka huu.
Mouringo amesema nyota huyo ameifanya safu yake ya ushambuliaji iwe kamili gado.
Remy anaweza kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Swansea leo baada ya kujiunga na Chelsea kwa ofa ya paundi milioni 10.5 kutokea klabu ya Queens Park Rangers.
Usajili huo ulitokana na kitendo cha Fernando Torres kujiunga na AC Milan kwa mkopo kwa miaka miwili iliyosalia katika mkataba wake.
Dili la kumsajili mshambuliaji huyo lilikuwa la mwisho kwa Mourinho na sasa ana chaguo la washambulaiji watatu, Remy, Diego Costa na Didier Drogba ambao waliwarithi Torres, Demba Ba na Samuel Eto’o, ambao walifunga mabao 19 tu katika michuano ya ligi kuu msimu uliopita.
“Remy amewasili na ni maisha mapya kwake,’” alisema Mourinho. “Kwa Fernando, pia ni maisha mapya kwake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Maisha yake hapa hayakuwa na mafanikio sana, lakini alikuwa na umuhimu na alitoa mchango mkubwa kwa klabu”.
“Tunampenda sana, lakini Remy ni miongoni mwa wachezaji tuliokuwa na malengo nao. Alikuwa ni mmoja wa wachezai tuliotaka kuwachukua kama milango itafunguliwa. Klabu yake ilikuwa tayari kutupa mshambuliaji huyo na sasa tuna washambuliaji watatu walio kamili”
Bosi huyo wa Chelsea hana wasiwasi kuhusu Remy licha ya ripoti kuwa alishindwa kufuzu vipimo vya afya Liverpool.
Ilielezwa kuwa nyota huyo ana matatizo ya moyo ambayo yaligundulika kwa mara ya kwanza alipojiunga na Marseille akitokea Nice mwaka 2010.