Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
KOCHA wa Yanga, Marcio Maximo amependekeza uongozi wa timu hiyo ya Jangwani umteme mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu utakaofunguliwa kesho na kufungwa Desemba 15, mwaka huu, imefahamika.
Mmoja wa ‘vigogo’ wa Yanga amekaririwa na baadhi ya mitandao ya michezo akieleza kuwa Maximo kabla ya kurejea nyumbani kwao, Brazil kwa mapumziko mafupi Jumatatu, ametoa pendekezo kwa uongozi kumtosa mkali huyo wa mabao kwa kuwa hayumo katika mipango yake.
Hata hivyo, kigogo huyo ambaye hakutajwa kwa jina, amesema Uongozi wa Yanga unaonekana kutoliafiki wazo la kocha huyo anayesaidiwa na Mbrazil mwenzake, Leonardo Leiva.
“Maximo amependekeza Kiiza aachwe, lakini wazo hilo hatujaliafiki, kuna sababu za msingi tumezingatia,” amekaririwa kigogo huyo huku akiweka wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa Kiiza akaendelea kuwamo kikosini.
Kiiza aliyefunga mabao 12 msimu uliopita, moja nyuma ya Mrisho Ngasa aliyekuwa kinara wa mabao Yanga, msimu huu amejikuta anasotea namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya Mbrazil huyo licha ya ukweli kwamba Mganda huyo ana kiwango kikubwa kuzidi mshambuliaji Mbrazil Geilson Santos Santana ‘Jaja’ anayeaminiwa mno na benchi la ufundi la Yanga kwa sasa.
Maximo alileta wachezaji wawili kutoka Brazil baada ya kutua Yanga mwishoni mwa Juni mwaka huu. Wachezaji hao ni kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Jaja ambao wamefunga bao moja kila mmoja msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Ujio wa Wabrazil hao, umemuondoa kabisa kwenye kikosi cha kwanza Kiiza, ambaye tangu amesajiliwa Yanga 2011, amekuwa akikubalika kwa makocha wote waliotangulia kabla ya Maximo.
Kiiza alisajiliwa Yanga wakati timu hiyo ya Jangwani ikinolewa na Mganda mwenzake, Sam Timbe, lakini akaendelea kuwa na nafasi kikosi cha kwanza hata kwa makocha waliofuatia, Mserbia Kostadin Papic, Mbelgiji Tom Saintfiet na Waholanzi Ernie Brandts na Hans van der Pluijm.
Maximo amerejea Brazil, akitoa mapumziko ya siku 10 kwa timu nzima, baada ya VPL kusimama kwa wiki saba kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Swaziland na Taifa Stars, usajili wa dirisha dogo, michuano ya Kombe la Uhai na mashindano ya Kombe la Chalenji ambayo hata hivyo inaonekana hayatafanyika baada ya waliokuwa wenyeji, Ethiopia kujitoa.
KAULI YA YANGA
Alipotafutwa na mtandao huu jijini Dar es Salaam leo mchana kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu amejibu kwa kifupi kwa kusema: “Rumours” (maneno ya kuzushwa).
“Mwalimu atajibu akirudi. Mwalimu pia bado hajaleta majina ya wachezaji anaowataka, akileta tutawafahamisha na hasa baada ya taratibu za usajili kukamilika,” ameongeza Njovu.
Imeelezwa leo na baadhi ya magazeti ya michezo kuwa Maximo ameamua kukatisha likizo yake na muda wowote atarejea nchini kwa ajili ya kufanya usajili wa dirisha dogo.