BAADA ya kuonekana kama kutulia kwa malumbano baina ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wakili na mdau mkubwa wa soka nchini, Damas Ndumbaro, aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amelichochea tena suala hilo, safari hii bungeni akihoji ukubwa wa makato na uhalali wa mgawo unaokwenda kwenye mfuko wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA).
Siku chake kabla ya kupigwa kwa mechi ya kwanza ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga msimu huu, TFF ilitangaza kuanzisha mfuko mpya ‘Jichangie’ kwa lengo la kusaka fedha kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana nchini ukitaka kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa klabu kutoka Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Kampuni ya Azam Media iliyonunua haki za matangazo ya televisheni ya mechi za Ligi Kuu.
Uamuzi huo ulipingwa vikali na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupitia wakili Ndumbaro ambaye ni daktari wa sheria. Malumbano ambayo baadaye yalisababisha TFF imfungie kwa miaka saba kujihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Huku hali ikionekana kutulia baada ya malumbano ya takriban miezi miwili, Rage analiibua suala hilo, tena akiwa ndani ya mjengo (bungeni) mjini Dodoma, ukumbi ambao umejaa watu wenye taaluma mbalimbali na wengi wao wakiwa ni wanasiasa.
Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisimama bungeni mjini humo Ijumaa ya wiki juzi na kutaka kama serikali ina habari ya makato ambayo klabu zinakatwa ni makubwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alisema DRFA kinanufaika kwa kupata fedha nyingi za makato ya mapato ya milangoni katika VPL bila kuwa na kazi yoyote.
Nkamia alisema DRFA wanapata fedha nyingi za mapato ya milangoni ambazo hazijulikani zinakokwenda wala kazi ambayo zinafanyia.
“Lazima tuchukue hatua,” Nkamia alisema huku akikiri makato yanayokatwa kwa klabu ni makubwa na kueleza kuwa awali alikutana na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), TFF na wadau wengine wa soka nchini kuangalia namna makato hayo yatakavyopungua.
“DRFA katika mechi moja wanapata mgawo mara mbili kwenye ile fomu ya mgawanyo wa mapato… na hawana kazi yoyote wanayoifanya zaidi ya kusubiri mapato.
“Sasa timu za vijana wanaohangaika ni TFF na serikali… lakini mapato yale yanayokatwa na makubwa kupita kiasi. Tumezungumza nao kuona njia za kuyapunguza.
“Leo ni timu kubwa mbili tu ndiyo zinaweza kuingiza mapato mengi… ni Yanga na Simba , Yanga ikicheza na Ndanda inaingiza mapato mengi sana kuliko Ndanda ikicheza na Stand United lakini makato bado ni yale yale.”
Makato ya ajabu ajabu, yasiyo na msingi na mengine mengi yanayofanana, ambayo yanabadilishwa-badilishwa majina tu licha ya kubeba maana moja, yameendelea kuzikamua hadi tone la mwisho klabu za Ligi Kuu katika kampeni “nzito” ambayo binafsi ninaona imedhamiria kuhakikisha haziendelei.
Mathalani, katika mechi iliyopita ya watani wa jadi, Simba na Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 18, zilipatikana Sh. milioni 427 lakini zaidi ya Sh. milioni 49 zilikatwa kinyonyaji na TFF kwenda mfuko mpya wa ‘Jichangie’ jambo ambalo linapingwa vikali na Ndumbaro ambaye kabla ya kutupwa jela ya soka, alikuwa mjumbe wa TPLB.
Katika mfuko huo mpya unaoonekana kumuumiza kichwa Rage, TFF ililamba Sh. milioni 24.77, Yanga walipata Sh. 17,339,700 na DRFA Sh. 7,431,300.
Mgawo mwingine wa mapato hayo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, ni Sh. milioni 43.67 ya uwanja, gharama za mchezo Sh. milioni 24.75, Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) Sh. milioni 23.29, TFF (ikapata mgawo mwingine) Sh. milioni 17.47, DRFA (nao wakalamba pesa nyingine) Sh. milioni 10.19, timu mwenyeji, Yanga (ikapata mgawo wa pili) Sh. milioni 100.46, timu ngeni, Simba ilipata Sh. milioni 71.34, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh. 65,176,932 wakati Sh. milioni 21.36 ilichukuliwa na CRDB kama asilimia tano ya gharama za tiketi.
Mambo ya msingi ya kujiuliza hapa ni vipi DRFA itengenezewe mwanya wa kupata mapato mengi kuliko klabu ilhali haina shughuli yoyote ya maana inayoifanya zaidi ya kusubiri mapato ya milangoni kama ilivyoelezwa na Nkamia? TFF wana maslahi yepi na chama hiki?
rage
Shirikisho linaonekana kuiweka kando Ilani ya Uchaguzi ya Rais wake wa sasa Jamal Malinzi iliyosisitiza kutetea mapato ya klabu na sasa imeyarudisha makato ya kinyonyaji ambayo kwenye Uwanja wa Taifa yalikuwa 17 kabla ya kufutwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala.
Makala, sasa Naibu Waziri wa Maji, alilazimika kutoa tamko la kuyafuta makato hayo Januari 22, mwaka jana baada ya NIPASHE kuchapisha ripoti iliyofichua ‘uozo’ uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji wa TFF kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa serikali huku baadhi yao wakijiita Wachina na kulamba Sh. milioni mbili kwa kila mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa.
Makato hayo yalikuwa: Maandalizi ya uwanja (pitch preparation), Uwanja (asimilia 10 sasa 15%), Usafi na ulinzi wa uwanja, Ulinzi wa mechi, Gharama za mchezo, Umeme (Sh. 300,000 kwa kila mechi U/Taifa), Wachina (stadium technical support) Sh. 2,000,000, Tiketi, Posho ya msimamizi wa kituo Sh. 120,000, Kamishna wa mechi Sh. 250,000, Waamuzi Sh. 440,000, Mwamuzi wa akiba, 70,000, Mtathimini wa waamuzi Sh. 254,000 (ilivyokuwa msimu uliopita), Kamati ya Ligi, FDF, DRFA na VAT.
Licha ya juhudi za wizara yenye dhamana ya michezo nchini kupunguza makato, vilio vimekuwa vikubwa sasa kwa sababu ni makato mengi mno yanayoua timu zetu changa ambazo zinahitaji sapoti ya serikali na TFF lakini suala hili linaonekana kufanywa kinyume na watendaji wa sasa wa shirikisho.
Miongoni mwa makato yanayochefua ni mgawo wa vyama vya soka vya mikoa husika hasa, DRFA ambao binafsi sijaona kitu cha maana kilichofanywa na chama hicho. Ninakumbuka baada ya gazeti hili kuhoji juu ya uhalali wa makato 17 ya kinyonyaji Uwanja wa Taifa, DRFA walionekana kushtuka na kuanda semina ya makocha jijini Dar es Salaam.
Makato wanayopewa DRFA ni ya nini na yanakwenda kufanyia kazi gani ikiwa kwa sasa vyama vya soka vya wilaya za Dar es Salaam (Kifa – Kinondoni, Tefa – Temeke na IDFA – Ilala) vyote vimeshapewa hadhi ya mikoa na vinaendesha ligi zao? Hiki ndicho Rage na wadau wa soka nchini wanataka wafafanuliwe kwa kina.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mwaka juzi kuwa makato hayo yanawaumiza na kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka klabu kuungana ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya klabu za soka nchini.
Naye Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele alizigeukia klabu kuwa zenyewe ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa TFF katika kupanga gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya gharama za mechi husika, hali ambayo mwishowe huwaacha wakiambulia fedha kidogo mno kutokana na mapato ya milangoni.
“Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa mzuri. Klabu hazina umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na malalamiko,” alisema Kahemele.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema shirikisho linalazimika kutoa fedha Sh. 200,000 kwa kila mechi inayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mafuta ya magari ya polisi.
Simba na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa Taifa kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na serikali iliwapoza kwa kuahidi kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, inaonekana hakuna juhudi za kulishughulikia suala hilo hivi karibuni, huku TFF ikianzisha makato mapya ya kinyonyaji baada ya serikali kuyafuta yaliyokuwa yanaihusu.
Katika ukokotozi wake, Ndumbaro alisema kama utaratibu wa ukataji makato ya milango utaendelea kama ulivyopangwa na Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kurudisha makato ya kinyonyaji, DRFA itakuwa inalamba fedha nyingi kuliko klabu za VPL kwa msimu.
Ikumbukwe kuwa marekebisho ya Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2014 yaliyosababisha kuongezwa kwa mfuko mpya wa ‘Jichangie’ yamefanywa na Kamati ya Mashindano badala ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, kinyume cha taratibu na Katiba ya shirikisho hilo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Ndumbaro.
 
Top