Mkude aliyekulia katika Kikosi B cha Simba, amesaini mkataba huo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kujiridhisha kuwekewa Sh. milioni 60 kwenye akaunti yake na Kamati ya Usajili ya Usajili ya Simba chini ya mwenyekiti wake, Zacharia Hanspope.
Kiungo huyo ambaye alikuwa amehusshwa na mipango ya makocha Mbrazil Marcio Maximo wa Yanga na Mcameroon Joseph Omog wa Azam FC katika kuimarisha vikosi vyao kipindi kifupi cha usajili (dirisha dogo) msimu huu, amekabidhiwa pia gari lake hilo ambalo lilinunuliwa na Simba siku moja kabla ya kuivaa Mtibwa Sugar katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao moja kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mkude amesaini mkataba huo mbele ya Hanspope huku Rais wa Simba, Evans Aveva akishuhudia.
Simba chini ya kocha aliyetua kwa mara ya tatu nchini kuinoa, Mzambia Patrick Phiri, imekuwa na mwanzo mbaya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuambulia sare katika michezo yote sita ya mwanzo kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting Jumapili.
Awali Simba ilikuwa imepanga kumsainisha Mkude mkataba wa miaka mitatu lakini imegonga mwamba kutokana na sababu ambazo hazijawekwa wazi, hata hivyo.