WATOTO 11 kutoka familia tofauti wamekamatwa mjini Singida, wakidaiwa kufanya vitendo vya ngono kwenye nyumba moja usiku wa kuamkia juzi.

Kikundi cha ulinzi shirikishi jamii, ndicho kilikamata watoto hao, wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 16, wa kike na kiume, wakiwa ndani ya chumba kimoja.

Inadaiwa kundi hilo la watoto, limeacha shule na kukimbia kwa wazazi wao, kisha kujiingiza kwenye vitendo vya mapenzi katika umri mdogo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bima, Salum Sudi alisema alipokea taarifa kuhusu watoto hao kutoka kwa mwenye nyumba walikokutwa.

Kwa mujibu wa Sudi, mwanamke huyo mmiliki anaishi jirani na nyumba hiyo, ambayo hutumiwa na mmoja wa watoto wake wa kiume kulala.

Mwenyekiti wa Mtaa alimkariri mama huyo, akisema alishtuka kutoka usingizini, kutokana na kelele za watoto hao usiku wa manane na akaenda kuita kikundi cha ulinzi shirikishi baada ya kujionea vitendo vichafu, vilivyokuwa vinafanyika.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mtunduruni, Petronila Katundu walikopelekwa watoto hao kwa ajili ya mahojiano zaidi, alisema hana cha kufanya, zaidi ya kuwaachia polisi wawachukulie hatua wazazi na walezi wa watoto hao.

Hata hivyo, wazazi na ndugu waliokuwepo eneo la tukio, walisema baadhi ya watoto hao wameshindikana na wameacha shule, kisha kuamua kujihusisha na vitendo vya mapenzi katika umri mdogo.

Tukio hili la baadhi ya watoto kuacha shule na kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo, limekuja huku takwimu za mkoa zikionesha kuwa zaidi ya watoto 20,000 wanaishi katika mazingira hatarishi mkoani Singida.

0 maoni:

Post a Comment

 
Top