MWALIMU WA MIAKA 30 AMUWEKA KINYUMBA MWANAFUNZI WAKE WA MIAKA 14
MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Sokoine, Manispaa ya Dodoma (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwekwa kinyumba na mwalimu wake David Macha (30).
Mwanafunzi huyo wa miaka 14 ni kati ya watoto wanaofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania kituo cha Tz 807 FPCT kilichoko Chamwino.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Jeshi la Polisi mkoani hapa, limelalamikiwa na wazazi wa mtoto huyo kwa kitendo cha kumlinda mtuhumiwa licha ya kupewa taarifa za uhalifu huo kwa zaidi ya miezi mitano sasa, limeshindwa kumchukulia hatua.
Uchunguzi wa Tanzania Daima ambao umethibitishwa na wazazi wa mwanafunzi huyo, umebaini kuwa mwalimu Macha amekuwa akifanya mapenzi na mwanafunzi huyo kwa zaidi ya miezi mitano sasa.
Wazazi wa mwanafunzi huyo wanathibitisha kuwa kwa zaidi ya miezi mitano, mtoto wao alikuwa na tabia ya kutoroka nyumbani nyakati za usiku na kulala nje, jambo ambalo lilianza kuwatia mashaka na kuanza kufuatilia nyendo zake.
Walidai kuwa wakati mwingine alikuwa akirudi nyumbani asubuhi kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule na anapoulizwa alikolala, alisema alikuwa katika mkesha.
Akisimulia mkasa huo, mjomba wa mwanafunzi huyo, Silas Mjengi, alisema binti yao anaishi na mama yake pekee katika eneo la Area ‘A’ mjini hapa baada ya mzazi huyo kutengana na mumewe.
Mjengi alisema kuwa baada ya kumbana binti yao, alikiri kufanya mapenzi na mwalimu huyo nyumbani kwake.
“Kwa muda mrefu nilipokea malalamiko toka kwa dada yangu juu ya vitendo vya mjomba wangu kuwa amekuwa akitoroka na kulala nje, ndipo nilipoamua kulifuatilia kwa umakini ikiwemo kumbana ambapo alikiri kuwa alikuwa anaishi na mwalimu kama mke na mume na hata kwenye simu yake alimwandika kwa jina la ‘my husband’,” alisema.
Kwa upande wake, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Esther Mjengi, alisema kuwa baada ya kuona tabia ya mwanaye imebadilika alianza kumfuatilia ndipo marafiki zake walipomueleza ukweli kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wake.
Alisema baada ya kufuatilia aliweza kumbamba akiwa nyumbani kwa mwalimu huyo kama mke wake na hata alipomfuata ili kuhojiana naye, aligoma kutoka ndani na ghafla alilazimika kuvua nguo na kumwachia blauzi ambayo alikuwa amevaa na kukimbia akiwa kifua wazi.
“Niliumizwa sana na mwanagu kujikita katika mapenzi na mwalimu, ukizingatia mwanagu bado ni mdogo na mwalimu ana miaka 30; wanangu naangaika nao sana kutokana na baba yao kutokuwa karibu nao, mbaya zaidi ni watoto ambao wanasoma kwa ufadhili wa Compassion Tanzania.
“Lakini baada ya kumbana alikiri kufanya ngono na mwalimu kwa zaidi ya miezi mitano sasa. Nilikwenda kushtaki kituo cha polisi cha kati Dodoma katika kitengo cha dawati la jinsia. Huweziamini! Sikutapa ushirikiano wowote; sijui nini kilifanyika kwani nilianza kubezwa badala ya kushughulikiwa na mtuhumiwa aliachiwa huru bila hata kuhojiwa,” alisema.
Tanzania Daima lilifanikiwa kuzungumza na mwanafunzi huyo, ambaye alikiri kuwa na uhusiano na mwalimu na kwamba alifikia uamuzi huo baada ya mwalimu huyo kumhudumia kwa vitu mbalimbali, ikiwemo kumpatia fedha.
“Aliahidi kunisaidia kwa kila kitu, kwani licha ya kunipa fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shuleni, lakini pia alikuwa akininunulia nguo zangu za ndani, pamoja na simu ya mkononi aina ya Tecno,” alisimulia bila woga.
Ofisa Elimu Manispaa ya Dodoma, Winfrida Bario, alikiri kupokea taarifa za tukio hilo, akisema kuwa alikaa nao wote mzazi na mwalimu, ambapo mwalimu na mwanafunzi walikiri makosa yao ya kuwekana kinyumba.
“Nilichoagiza kwa polisi ni kuhakikisha hatua zinachukuliwa dhidi ya mwalimu huyo kwani moja kwa moja amevunja kanuni na taratibu za kazi na hata kama ingekuwa vipi mwalimu huyo tayari ameishamharibu kisaikolojia mwanagunzi huyo.
“Mwanafunzi huyo yuko darasa la saba unafikiri anaweza kuwa na akili nzuri tena maana ameishamharibia kila kitu. Mbali na hili, kwa mwalimu wa miaka 30 kutembea na mwanafunzi wa miaka 14 ni kosa la ubakaji,” alisema ofisa elimu huyo.
Aliongeza kuwa kitendo hicho ni cha aibu kwani mtumishi wa umma hapaswi kukiuka maadili ya utumishi wake.
Naye mwalimu ambaye alibambwa kwa kosa hilo la kumweka mwanafunzi kinyumba alijitetea kuwa alifanya hivyo kutokana na tamaa za mwili lakini si tabia yake.
“Ni kweli nilikuwa naishi na mwanafunzi huyo lakini mimi si tabia yangu bali shetani alinipitia, nimewaomba radhi wazazi wa mtoto wanisamehe sitarudia tena na nasubiri kama watanisamehe ila sikutarajia kabisa,” alijitetea.
Upande wa jeshi la polisi umeonekana kuwa na kigugumizi kwani hakuna ufafanuzi wowote wa kina uliotolewa licha ya mzazi wa mtoto kuonyesha vielelezo vyote vya polisi na daktari kuhusiana na mtoto wake kutendewa vitendo vya ngono na mwalimu huyo.
Kamanda wa polisi mkoa Dodoma, David Misime, hakupatikana kulizungumzia tukio hilo lakini ofisa habari wa jeshi hilo, Kung’alo Lupy, alisema suala hilo linaendelea kufanyiwa uchunguzi.
0 maoni:
Post a Comment