SIRI ZA MKATABA WA MRISHO NGASSA NA KLABU YA SIMBA SC
WAKATI Mrisho Ngassa amepitishwa kuichezea Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, imedhihirika kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliupokea mkataba wa Simba tangu Desemba 17, mwaka jana.
Mwanaspoti limeuona mkataba wa Simba na Ngassa, ambao umegongwa muhuri wa TFF kuonyesha kuwa ulipokelewa katika shirikisho hilo tangu Desemba 17 mwaka jana.
Mkataba huo, unaonyesha kuwa Ngassa alisaini kuichezea Simba Agosti 2, mwaka jana na kwamba ulitakiwa uanze kutumika Mei 22 mwaka huu na kumalizika Mei 31 mwakani.
Katika moja ya makubaliano kwenye mkataba huo, Ngassa haruhusiwi kuichezea Yanga katika kipindi hicho au timu nyingine yoyote na mshahara wake ungekuwa Sh2 milioni kwa mwezi.
Hata hivyo katika kikao chake cha mwishoni mwa wiki, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Soka (TFF), chini ya Alex Mgongolowa ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga, lakini ikamfungia mechi sita pamoja na kumtaka arejeshe Sh30 milioni ambazo alichukua Simba pamoja na asilimia hamsini ya fidia ambazo ni Sh15 milioni.
Kamati hiyo ilibaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) na anatakiwa kurejesha fedha alizopokea Msimbazi Sh30 milioni pamoja na fidia ya asilimia 50 (Sh15 milioni) ya fedha hizo hivyo kufanya awe anadaiwa Sh 45 milioni.
Kamati hiyo pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii Jumamosi iliyopita), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Hiyo ina maana kuwa Ngassa amekosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam na nyingine tano za Ligi Kuu Bara ambazo ni dhidi ya Ashanti, Coastal Union, Mbeya City, Prisons na Azam.
Kwa mara ya kwanza, Ngassa ataonekana katika Ligi Kuu Bara, Yanga itakapocheza dhidi ya Ruvu Shooting Septemba 28 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
0 maoni:
Post a Comment