Baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 na Yanga, kikosi cha Simba kesho jioni kitashuka katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kuvaana na Coastal Union ya mjini humo.
Kikosi cha Simba kiliwasili Tanga jana mchana tayari kwa mchezo huo utakaochezwa kesho saa 10:00 jioni na tayari shamrashamra zimeshaanza kutawala jiji la Tanga.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekile Kamwaga ameuambia mtandao huu kwamba, kikosi cha Simba kiliwasili salama jana jijini Tanga tayari kwa mchezo huo wa kesho na wachezaji Hnery Joseph, Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud hawapo katika kikosi hicho.
“Timu imefika salama Tanga tangu jana mchana na hali ya kikosi kizima ni nzuri kinachosubiriwa sasa ni muda kufika ili tuweze kutazama pambano hili safi na la kuvutia kwetu sote, kwani Coastal ni timu nzuri ambayo ina wachezaji kadhaa ambao wamewahi kuwika na klabu mbalimbali za hapa nchini.
“Sisi kama Simba tunaamini tuna timu nzuri ambayo inaweza kupambana na timu yoyote na kutwaa ubingwa hivyo wakazi wa Tanga na miji ya jirani wajitokeze kwa wingi uwanjani kutazama pambano hili la kuvutia,” anasema Kamwaga.
Naye Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora amesema kikosi cha timu yake kimejiandaa vya kutosha na hakuna tatizo lolote linaloikabiri timu yake kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Simba.
“Sisi tupo vizuri kabisa tunaisubiri Simba kwa hamu kubwa kuweza kupambna nao kwani tumejiandaa vizuri chini ya kocha wetu Joseph Lazaro ambaye amejiunga nasi hivi karibuni akichukua nafasi ya Ahmed Morocco.
“Tuna wachezaji wengi wazuri ambao wamewahi kutamba na timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, tunachohitaji sisi ni kufanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” anasema Aurora.
Wachezaji wa Simba waliowahi kuichezea Simba ni Haruna Moshi ‘Boban’, Juma Nyosso, Jerry Santo na Pius Kisambale ambaye pia amewahi kuichezea Yanga. Wachezaji wa Yanga waliowahi kuichezea Yanga ni Razack Khalfan, Atupele Green, Shaaban Kado na Kisambale.  

0 maoni:

Post a Comment

 
Top