HAMAD Yahya ameibuka mshindi wa uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) uliofanyika leo Oktoba 25 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower kuanzia saa 3 asubuh.
Kwa mujibu wa habari zilizotufikia hivi punde, Yahya anayetokea Mtibwa Sugar ameshinda kwa asilimia 100.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.
“Ombi langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.
Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.
“Ajenda yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.
Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.
0 maoni:
Post a Comment