UCHAGUZI wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) unafanyika leo Oktoba 25 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower kuanzia saa 3 asubuhi.
Mgeni rasmi katika uchaguzi huo wa Bodi ya TPL ambao unafanyika kwa mara ya kwanza atakuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Viongozi wa klabu za FDL wamefikia hoteli ya Royal Valentino iliyoko Barabara ya Uhuru wakati wale wa VPL ambao pia watashiriki Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wamefikia hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo.
Kitu cha kushangaza na kufurahisha katika uchaguzi huo ni kwamba nafasi nyingi zinawania na mtu mmoja mmoja tu, hivyo mpiga kura atakuwa na kazi ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
Hii ina maana kwamba, kuna uwezekano mdogo wa wagombea hao kushindwa na hata kama ikitokea mmoja ameshindwa, waliochaguliwa wataendelea na uongozi huku nafasi hiyo ikizibwa baadaye.

0 maoni:

Post a Comment

 
Top