Ndugu Leodegar Tenga
Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin Ndolanga Mwenyekiti
mstaafu wa
iliyokuwa
FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukupongeza Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar
Tenga na Kamati yako ya utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia
haitawasahau. Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika
ndani na nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa mrefu. Wapo walioshinda
na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja tu kujenga mpira. Kama
tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu kimoja, tuinyanyue soka yetu.
Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia madarakani alfajiri ya
tarehe 28-11-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi. Nitaelezea changamoto
chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
1.
Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali
ya kimataifa. Mfano ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji
wiki ijayo, Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano
ya Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya
yanahitaji maandalizi ya haraka.
2.
Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea
azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019.
Jambo hili tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na
timu nzuri ya kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho
kuunda timu ya Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya
vijana tutakayoiandaa sharti ijielekeze
kwenye ratiba hii.
3.
Udhamini wa timu za vijana na za
wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF.
Timu zetu za Taifa kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni
brands inabidi ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa
hizo timu. Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto
hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani anategemea
matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende kwa wadhamini
tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu zetu.
Tusisubiri waje tuwafuate sisi.
4.
Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike
kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant)
atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili
tuwekeze kitega uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa
zenye nembo yetu zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki
yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee
suala la fujo viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa
mwamuzi unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha
nyuma ya kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya
makusudi au ya bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mechi
ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za FIFA, CAF na TFF ziko wazi na
adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika kucheza kwenye uwanja
mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au
kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu
Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya
na Dar es salaam wote tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema
iwe mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya
kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye
ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao.
Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za mashabiki
ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili. Viongozi wa klabu
na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi
katika kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizi tunao na tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote
kuanzia Serikali, Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina
imani tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira
kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.
0 maoni:
Post a Comment