Mlinda mlango namba moja nchini Juma Kaseja Juma leo ameanza rasmi mazoezi na timu yake mpya wa Young Africans katika uwanja wa Bora Mabatini - Kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa.
Kaseja ambaye amesajiliwa na Young Africans kipindi cha dirisha dogo ataitumikia timu yenye makao makuu yake mitaa ya Twiga/Jangwani kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mwaka 2015 mwezi wa Disemba.
Mara baada ya kufika mazoezini leo asubuhi Kaseja alipokelewa na kocha mkuu Brandts, kocha msaidizi Minziro pamoja na wachezaji wenzake wa Yanga, huku golikipa Ally Mustapha "Barthez" akimuongoza katika mazoezi yao ya magolikipa chini ya usimamizi wa kocha wa makipa Razak Siwa.
Kocha wa makipa Razak Siwa amesema ujio wa Kaseja ndani ya Yanga ni mzuri, kwani kwa sasa ana magolikipa wanne wote wenye uwezo wa hali ya juu, hivyo jitihada za mchezaji ndio zitakazompa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.
Kikosi cha Young Africans kinaendelea na mazoezi wiki ya pili sasa katika uwanja wa bora-mabatini Kijitonyama ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mzunguko wa pili, mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na mchezo wa hisani wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013.