Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam

WAGONGA nyundo wa Mbeya,  Mbeya City FC wameanza mazoezi yao leo hii kuwawinda wana Lambalamba, Azam fc aprili 13 mwaka huu katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa dimba la kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Taarifa iliyotolewa na afisa habari wa klabu hiyo, Freddy Jackson imeeleza kuwa mazoezi ya leo yamekwenda vizuri na malengo yao ni kuibuka na ushindi katika dimba lao la nyumbani ambalo hawajawahi kufungwa tangu waanze ligi kuu msimu.
Wakati huo huo, kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi ameueleza mtandao huu kuwa wao walijiandaa kwa mechi zote 26 za ligi, hivyo mchezo ujao dhidi ya Azam fc watapambana kusaka pointi tatu muhimu.
“Ligi imekuwa ngumu sana msimu huu. Kila klabu imejipanga kutafuta matokeo. Lakini mimi siwezi kuwaahidi mashabiki lolote zaidi ya kusubiri mechi yenyewe. Cha msingi waendelee kutuunga mkono zaidi ili kufikia malengo yetu”. Alisema Mwambusi.
Kocha huyo aliyejijengea jina kubwa baada ya kuchachafya msimu wake wa kwanza wa ligi kuu akiwa na Mbeya City, aliongeza kuwa matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Ashanti United ambapo walitoka suluhu pacha ya bila kufungana yaliwaharibia kwa kiasi kikubwa katika mbio zao za kuwania ubigwa.
“Nilisema toka mwanzo kuwa mechi ya Ashanti ingekuwa ngumu kwetu. Mazingira ya uwanja wa ugenini si sawa na nyumbani”.
“Pia mazingira ya Ashanti ambao wanakwepa kushuka daraja yaliufanya mchezo uwe na presha kubwa kwa upande wetu, lakini tunajipanga dhidi ya Azam fc”. Alisema Mwambusi.
Rasmi Mbeya City baada ya kutoka suluhu pacha dhidi ya Ashanti United,  walishajitoa kuwania ubingwa, huku wakiwaombea mabaya Yanga wasifanye vizuri mechi zao tatu ili waambulie nafasi ya pili.
Mpaka sasa City wapo nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 24 na kusaliwa na mechi mbili tu mkononi.
Kama watashinda mechi zote watafikisha pointi 52 ambazo Yanga wanaweza kuzivuka katika mechi zao tatu walizosaliwa nazo.
Kama Mbeya City wanahitaji nafasi ya pili wanatakiwa kuwaombea Yanga watoe sare mbili na kupoteza mechi moja ili wafikishe pointi 51 ambazo wataweza kuzivuka kama watashinda mechi mbili walizonazo mkononi mwao.
Hata hivyo inaonekana kutokuwa rahisi kwa Yanga kutoa sare mechi mbili kwasababu ya ubora wao.
Ingawa kwenye mpira lolote linaweza kutokea, lakini bado Yanga wanaonekana kuwa na uchu mkubwa zaidi katika mechi zilizosalia kuanzia ya jana ambayo walishinda mabao 5-1 dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.
Yanga wanatarajia kukutana na Kagera Sugar jumatano ya wiki hu  uwanja wa Taifa, na baada ya hapo watasafiri kwenda Arusha kuwafuata JKT Oljoro na kufunga pazia la ligi kuu dhidi ya Simba sc uwanja wa Taifa Aprili 19 mwaka huu.
Nafasi inayoonekana kuwa wazi kwa Mbeya City ni ya tatu.
Na kama wataambulia hiyo,  haitakuwa mbaya kwao kwani ni msimu wao wa kwanza.
Hata hivyo itawauma kwasababu walikuwa na mategemeo makubwa japokuwa wameshindwa kuyafikia kutokana na ushindani wa timu zote.

Mechi ijayo wanacheza na Azam fc na baada ya hapo watamalizia kibarua chao na Mgambo JKT Aprili 19 mwaka huu uwanja huo huo wa Sokoine.
 
Top