JOSE MOURINHO amebainisha kuwa anataka kuwapumzisha Wachezaji kadhaa muhimu watakaposafiri kwenda Anfield hapo Jumapili kucheza na Vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool, kwenye Mechi muhimu mno kuamua nani Bingwa.
Liverpool wako Pointi 5 mbele ya Chelsea huku Gemu zikiwa zimebaki 3 kwa Timu hizo na Mourinho anataka kutilia mkazo Gemu yao ya Marudiano na Atletico Madrid ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI itakayochezwa Stamford Bridge baada kwenda Sare 0-0 huko Estadio Vicente Calderon Jijini Madrid Jumanne Usiku.
Mourinho amenena: “Nitachezesha Wachezaji ambao Jumatano hawatacheza na Atletico!”
Baada ya kufungwa Bao 2-1 na Sunderland Wikiendi iliyopita, Chelsea wamebakia na nafasi finyu ya Ubingwa na hata wakiwafunga Liverpool bado watabaki nyuma yao.
Lakini, Manchester City, ambao wana Mechi mbili mkononi ukilinganisha na Liverpool na Chelsea, wanaweza kutwaa Ubingwa kwa tofauti ya Magoli ikiwa watashinda Mechi zao 4 na Liverpool kupoteza Mechi 1.
Mbali ya Mourinho kusema atabadili Wachezaji wakicheza na Liverpool, wao wanakabiliwa na Majeruhi baada ya John Terry na Kipa Petr Cech kuumia kwenye Mechi na Atletico na inasemekana watakuwa nje kwa muda huku pia wakiwakosa Frank Lampard na John Mikel Obi kwenye Marudiano na Atletico baada ya kuzoa Kadi za Njano na hivyo kufungiwa kutocheza Mechi hiyo.
Pia, Chelsea haiwezi kuwatumia Nemanja Matic na Mohamed Salah kwenye Mechi na Atletico kwa vile hawaruhusiwi kucheza na UEFA.
Hivyo, Mourinho yuko huru kuwachezesha Lampard, Obi, Matic na Salah kwenye Mechi na Liverpool bila kuathiri mipango yake ya Gemu na Atletico.
Vilevile, Mourinho amelalamikia sana uamuzi wa wao kucheza na Liverpool Jumapili wakati Jumatano wana Mechi muhimu na Atletico Madrid na badala yake alitaka Mechi hiyo kuchezwa Jumamosi.
 
Top