DSC_4852
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga SC, Tukuyu Stars na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars, Seklojo Johnson Chambua amewapongeza Azam fc kwa usajili wanaoendelea kuufanya ili kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
Chambua amesema usajili huo ni jambo lenye sura mbili tofauti ambapo upande wa kwanza ni kwa Yanga na wa pili kwa Azam fc.
“Kwa mashabiki wa Yanga wameumia kwasababu wameondokewa na wachezaji wao, lakini kwa upande wa Azam wamefurahi kwasababu wameimarisha kikosi chao”.
“Azam watakuwa wanaiwakilishi nchi katika michuano ya klabu bingwa Afrika mwakani, kwahiyo wapo katika kuimarisha kikosi chao”.
“Taswira ya Azam kusajili si kuikomoa timu yoyote bali ni kuimarisha kikosi chao. Inawezekana wanasajili kuimarisha kikosi na siamini kama wanawakomoa Yanga”.
“Nadhani Yanga nao wanahitaji kujipanda kwa ajili ya kombe la shirikisho, lakini kwa wachezaji hawa kuondoka inawezekana ni matakwa yao binafsi”. Alisema Chambua.
Akizungumzia jinsi Domayo atakavyosuka kiungo cha Azam na Salum Abubakar `Sure Boy`, Sekloja alisema wachezaji hawa wanafahamiana kwasababu wamecheza timu ya Taifa kwa muda mrefu hivyo watakuwa msaada mkubwa kwa klabu yao.
“Sure boy na Domayo japokuwa walikuwa wanacheza timu tofauti, lakini wamekutana mara nyingi timu ya taifa. Nadhani itakuwa rahisi kwa kocha Omog kuwachezesha pamoja”. Aliongeza Sekloja.
 
Top