1044693_168325606678827_260852630_n
Na Baraka Mpenja, Dar es Salaam
KIUNGO mshambuliaji wa Mbeya City fc, Deus Kaseke amefungua milango kwa klabu yoyote inayotaka kumsajili kwa masharti ya kumlipa maslahi mazuri zaidi.
Kaseke ameueleza mtandao huu kuwa mpira ni kazi yake na atacheza sehemu atakayopata maslahi makubwa zaidi ya yale anayopata katika klabu yake ya Mbeya City fc.
“Hakuna anayeridhika na kile anachopata, kila kukicha unaomba upate zaidi.”
“Ikitokea klabu yenye dau nono kunihitaji, naondoka zangu”. Kaseke amezungumza na mtandao huu.
“Mtazamo wangu mimi uko hivi, kama ikitokea timu yoyote itakayonihitaji mimi, nafungua milango na waje wamalizane na klabu yangu”.
“Kama Mbeya City wataridhia niondoke nitafanya hivyo,kama watakataa sitaweza kulazimisha kwasababu nina mkataba nao, lakini watatakiwa kuongeza mambo `fulani`”.
Kaseke amekuwa akitajwa kuwa katika mipango ya kocha wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic na inasemekana katika ripoti yake aliyokabidhi kwa viongozi kabla ya kwenda kwao kwa mapumziko, ameagiza nyota huyo asajiliwe.
Akizungumzia tetesi za kuwindwa na wekundu wa msimbazi Simba sc, Kaseke alisema hakuna mchezaji asiyependa kuchezea klabu kubwa kama hiyo na wakija na mambo anayoyahitaji atajiunga nayo kwasababu anatafuta maisha.
“Kama Simba wananihitaji wameona naweza kufiti katika mfumo wao, kama ikitokeoa nitaenda na kupigana kupata nafasi”. Aliongeza Kaseke.
Kaseke alisema kwa sasa yuko likizo, lakini jumatatu ya wiki ijayo anaanza mazoezi binafsi ya kujiweka fiti kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Kuhusu nafasi ya tatu waliyoshika msimu uliopita, Kaseke alisema walikuwa wageni lakini walijitahidi kwenda sambamba na kasi.
Nyota huyo aliongeza kuwa msimu ujao wataendeleza pale walipoishia na kutwaa ubingwa au nafasi ya pili ili kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
 
Top