Nje? Luis Suarez anaweza kukosa fainali za kombe la dunia baada ya kubainika kuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti.
Balaa kubwa: Suarez anaweza kukosa mechi zote za hatua ya makundi.
MSHAMBULIAJI hatari wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez yuko hatarini kukosa fainali za kombe la dunia baada ya kugundulika kuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti kutokana na majeruhi aliyoyapata katika mazoezi ya jana jumatano.
Nyota huyo aliyeing`arisha Liverpool na kushika nafasi ya pili ya ligi kuu soka nchini England msimu uliopita anaweza kukaa nje ya uwanja kwa wiki nne au sita.
Hizi ni taarifa nzuri kwa England ambao wamepangwa kundi D katika fainali za mwaka huu nchini Brazil.
Ripoti kutoka Uruguay zinaeleza kuwa Suarez yuko hatarini kukosa mechi zote za hatua ya makundi baaada ya kipimo cha MRI kuonesha kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka leo hii.
Taarifa rasmi kutoka chama cha soka cha Uruguay alisema: ‘Haikutarajiwa hata kidogo. Taarifa za mwisho ni kwamba tumeshaamua cha kufanya, lakini kuna uwezekano mkubwa akafanyiwa upasuaji”.
“Hatuwezi kusema lolote. Shirikisho la soka litatangaza taarifa rasmi alhamisi asubuhi (leo)”.