Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu) kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Washambuliaji hao watatokea moja kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.
Ujio wa washambuliaji hao utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa wamepatikana kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo fainali zake zitachezwa mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wan je ambaye tayari ameripoti Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya FIFA.
Naye Kocha Nooij atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Accomondia.
Wakati huo huo, Zimbabwe inawasili usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara wa watu 27. Timu hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam.
Zimbabwe itafanya mazoezi siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo.