Viongozi wa Matawi ya Yanga wakiongozwa na Mohamed Msumi (wa kwanza kulia) . Picha na Gervas Mwatebela
WAKATI kwa ridhaa yao wanachama wa klabu ya Yanga waliamua kuuongezea muda wa mwaka mmoja uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti wake, Yusuf Manji, huku baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakitofautiana na maamuzi hayo, viongozi wa matawi wameutaka uongozi kuwachukulia hatua wanachama na viongozi wa Matawi wanaochochea vurugu katika klabu hiyo kwa mujibu wa katiba na miongozo ya klabu hiyo.
Wakizungumza leo, viongozi hao wamewaonya baadhi ya wanachama ambao wamekuwa wakiongelea masuala ya klabu hasa ya kiutawala pasipo kupata ruhusa ya mwenyekiti na kuchafua hali ya hewa ndani ya klabu hiyo kuacha mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua kwani kanuni zipo wazi kwa sababu wanatakiwa kutoa maoni yao kupitia mkutano mkuu na vikao halali ama kwa ruhusa ya mwenyekiti wa klabu hiyo Yusufu Manji.
Baadhi ya wanachama wamekuwa wakipinga maamuzi yaliyopitishwa na klabu hiyo katika mkutano mkuu uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu wa kumuongezea mwaka mmoja Yusufu Manji ili aweze kutekeleza malengo aliyojiwekea kitendo kinachodaiwa kwenda kinyume cha katiba ya klabu ya Yanga .