Mtadanganyika?: Wanachama wa Simba jiepusheni na siasa nyepesi za wagombea. Tumieni muda kutafakari sera za wagombea.
Na Baraka Mpenja, Dar es Salaam
0712461976
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
Hata hivyo, TFF inawahimiza wanachama wa klabu ya Simba kuwa watulivu na wafanye uchaguzi wao kwa amani.
Taarifa hizi kwa asilimia 100 ni njema kwa wanachama, mashabiki, viongozi, wafadhili na wadhamini wa klabu ya Simba sc.
Watu wote wanaopenda ustawi wa mpira wa nchi hii walitegemea busara za Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi ambaye alitangaza kusimamisha uchaguzi huo jumapili iliyopita. Kauli yake ilizua utata miongoni mwa wanasimba na yakazungumzwa mengi, lakini usikivu wa Malinzi umefanikisha ndoto za Wanasimba kupata viongozi wao juni 29.
Juhudi za Rais wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage zimewasha taa ya kijani kwa Simba baada ya kumuomba Malinzi maandalizi ya uchaguzi yaendelee na hatimaye kufanyika juni 29 kama ulivyopanga. Ingekuwa mbaya kama uchaguzi usingefanyika siku hiyo kwasababu klabu inahitaji viongozi ili usajili uanze na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.
Zoezi linalosubiriwa kwasasa ni kuzinduliwa kwa kampeni ili kila mgombea anadi sera zake na kuwajulisha wanasimba kwanini anaomba nafasi ya uongozi.
Nafasi mbili za juu, Urais na makamu wa Rais zinavuta hisia za wanachama wengi, lakini kuondoshwa kwa Michael Richard Wambura, kumewaacha Evance Aveva na Andrew Tupa kupambana.
Safari ya kuenguliwa kwa Wambura ilikuwa na mizengwe mingi na ilisababisha mvutano mkubwa ndani ya klabu ya Simba, lakini mwisho wa siku sheria na kanuni zimetoa jibu.
Ni imani yangu kuwa utulivu utakuwepo na wale waliokuwa wanamuunga mkono Wambura watakuwa wavumilivu kwasababu kila unaposhindana lazima ukumbuke kuna kushinda na kushindwa.
Tatizo la watu wengi wanawaza kushinda tu, lakini kushindwa wanaona kama ni dhambi. Penda kushindwa, halafu jipange upya. Ukiwa mtu wa kuwaza kushinda tu, ukishindwa `unapaniki` na hatimaye kushindwa kabisa kabisa!.
Wanachama wa Simba mnatakiwa kuvunja kundi la Wambura na kushirikiana kwa pamoja ili juni 29 mpate mtu atakayewaunganisha na kuifanya Simba kuwa imara. Naamini uchungu mlioupata kwa miaka miwili sasa unatosha na kuna haja ya kuijenga Simba ya ushindani.
Kwa kuanzia, lazima mpate viongozi sahihi, wenye mtazamo sahihi na watakowafanya mpige hatua kwenda mbele.
Kampeni zinaanza juni 24 mwaka huu kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na kamati ya uchaguzi chini ya wakili, Dkt. Damas Daniel Ndumbaro.
Niwakumbushe kitu kimoja tu,kampeni ni nafasi ya mgombea kunadi sera, mipango na kueleza kwanini anagombea. Pia anaweza kueleza jinsi atakavyotekeleza sera zake na kufanikiwa.
Katika chaguzi za kidemokrasia, Kampeni ndio muda unaowafanya watu wapate viongozi bora na bomu. Hapa ndipo siasa ilipolalia. Ushawishi huwa ni mkubwa na kudanganywa pia kupo.
Mara nyingi, wagombea wengi wanapenda kuongea mambo yanayovutia na kushawishi. Usipokuwa makini unaweza kumchagua mtu mwenye maneno mazuri, lakini ikifika wakati wa utekelezaji, mambo yanageuka.
Najua kwa muda wote huu, wagombea wote wamekuwa wakiandika na kuandikiwa cha kuzungumza mbele ya wanachama wa Simba. Najua yatazungumzwa mengi kutoka kwa wagombea, lakini umakini wa wanachama ndio utachambua mtu sahihi wa kumpa kura.
Rais wa Simba anayemaliza muda wake, Ismail Aden Rage amefanya juhudi kubwa kuhakikisha anaondoka madarakani juni 29 mwaka huu kwa kuwasiliana na Rais Jamal Malinzi aliyetangaza kusimamisha uchaguzi wa Simba.
Wapo watakaosema lazima wajenge uwanja wa kisasa, wauze jezi za klabu kwa faida ya timu, wataifanya klabu kuwa bora uwanjani kwa kusajili wachezaji wazuri, kuifanya Simba ijitegemee na mengine mengi.
Sina shaka na mtu atakayesema haya kati ya mengi yatakayosikika. Najua kweli Simba inahitaji mambo kama hayo na mengine mengi.
Lakini mwisho wa siku, kuna kitu kinaitwa `sera au ahadi zisizotekelezeka`. Hapa lazima wanachama wa Simba kuwa makini ili msije kujenga imani kubwa na mgombea fulani kwasababu ya sera zake, kumbe hazitekelezeki.
Lazima upime uwezo wa klabu yenu kifedha, halafu pima uwezo wa mgombea anayezungumza, halafu dadavua kama kweli anaweza kufanikiwa anayozungumza.
Sisemi uwezo wa kifedha hapa, nazungumzia utashi, uimara na ujanja ujanja wa kutafuta njia za kupata fedha kwa faida ya Simba. Mgombea mwenye uwezo wa kuhangaika kwa ajili ya klabu kwa kuzungumza na makampuni, wadhamini na wafadhili ili aitunishe akaunti ya timu kwa matumizi tofauti tofauti.
Moja ya siri ya kufanikiwa kwa kiongozi ni kuchagua mambo machache kwa muda ulionao na kuyatekeleza ipasavyo. Lakini kwa siasa za Tanzania, mgombea anaahidi mambo 10 anatekeleza matatu au hatekelezi yote. Ikifikia wakati wa uchaguzi anajipanga na uongo mwingine.
Kiongozi bora ni Yule anayekuwa na malengo machache ndani ya muda mfupi. Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi, anajikita kwenye ahadi zake chache na akiweza, atajijengea heshima.
Wanachama wa Simba, pimeni sera za wagombea wenu na kuzichambua kama zinatekelezeka. Msije mkajidanganya na kuwaamini kwa maneno ya mdomoni, lakini kiuhalisia hayawezekani.
Wapo watu kazi yao ni kuandaa sera za wagombea. Wana uwezo mkubwa wa kuandaa mipango yenye mvuto, lakini utekelezaji wake unakuwa mgumu kwasababu wanaandika tu bila kuangalia mazingira ya pale wanapoenda kuongoza.
Maneno si kigezo cha kumuamini mtu, lazima ujua anawezaje kufanikiwa kwa mazingira mliyonayo kwenye klabu.
Kwa wagombea, ogopeni kudanganya watu wazima. Kama kweli mna nia ya dhati kuindeleza klabu ya Simba, njooni na sera zinazotekelezeka na ambazo zipo chini ya uwezo wenu. Sio mnakuja na mambo mazito ambayo Simba haiwezi kuyabeba.
Kama mtadanganya na kushindwa kufikia malengo yenu, mjiandae kuingia katika orodha ya wanasiasa waliovamia mpira bila kuwa na nia ya kweli. Ni imani yangu kuwa mmeomba nafasi kwasababu mnataka kufanya kazi nzuri.
Simba inahitaji mabadiliko baada ya kupitia kipindi kigumu cha miaka miwili. Kila atakayepewa nafasi, basi awajibike vizuri.
Wanachama wa Simba, juni 29 mna mamlaka makubwa kikatiba. Ninyi ndio mtashika rungu na kuamua nani anaingia nani anatoka. Msichague kwa kushawishika na wenzenu.
Kura ni siri ya mtu na lazima iwe siri. Kama mtu anatoka ndani ya chumba cha kupigia kura anatakiwa aendelee na mambo yake, sio anamwambia mwenzake, mimi nimemchagua fulani, nawewe kumchague. Kila mtu aingie kivyake na kufanya yake
Kila la heri wana Simba kuelekea uchaguzi wenu wa Juni 29. Amani na iwe nanyi kwa wakati huu muhimu.