Shujaa wa penati: Sergio Romero alidaka penati ya Ron Vlaar katika ushindi wa penati 4-2 dhidi ya Uholanzi.
NDOTO za Argentina kutwaa kombe la dunia mwaka huu katika ardhi ya majirani zao Brazil zimeendelea kuwepo baada ya kuipiga Uholanzi kwa mikwaju ya penati 4-2 usiku huu.
Mechi hii kali ya nusu fainali ya pili imekwenda mpaka dakika 120, lakini matokeo yalisimama 0-0.
Mlinda mlango wa Agrgentina, Sergio Romero alikuwa shujaa baada ya kuokoa penati mbili za Ron Vlaar na Wesley Sneijder.
Waamerika kusini hao walifunga penati zao zote nne na sasa watacheza fainali dhidi ya Ujerumani, siku ya jumapili katika dimba la Maracana.
Katika mchezo wa leo, Lionel Messi alibanwa na wachezaji wa Uholanzi na kushindwa kuleta madhara.
Naye Robin Van Persie alifichwa kabisa na alitolewa katika dakika za nyongeza.