KABURU
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MAKAMU wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange `Kaburu` ni miongoni mwa watu wenye mtazamo sahihi katika soka la vijana nchini Tanzania.
Inawezekana ana mapungufu yake kama ilivyo kwa mtu yeyote, lakini mara zote mtazamo wake wa kuendeleza soka la vijana katika klabu ya Simba unanivutia sana.
Ili kutengeneza mfumo na falsafa ya klabu, huwezi kukwepa soka la vijana. Timu kama Barcelona zilianzisha mpira wa aina ya `Tiki -taka` . Huu ni mfumo wa kucheza mpira kwa kumiliki maeneo yote muhimu ya uwanja.
Mpira huu huwa wachezaji hawasimami eneo moja kama ilivyo kwa mifumo mingine. Wachezaji wanatakiwa kubadilishana nafasi kadri wawezavyo. Mlinda mlango pekee ndiye mchezaji anayebaki eneo moja.
Katika mfumo wa `Tiki-Taka`, beki anaweza kuwa mshambuliaji, kiungo anaweza kuwa beki, mshambuliaji anaweza kuwa beki ndani ya uwanja. Yaani kama beki wa kati amepanda, kiungo wa kati anarudi kukaba nafasi yake. Kama beki wa kulia amepanda kupandisha mashambulizi, winga wa kulia anaweza kushuka katika nafasi ya kulia kuzuia.
Ninachojaribu kusema ni kwamba kwenye mpira wa `Tiki-taka`, hakuna kukaa nafasi moja, yaani kama ni namba tisa unaweza kuwa mlinzi kwa muda wowote uwanjani au beki unaweza kushambulia .
IMG_1687Ramadhan Singano `Messi` (kulia) ni zao la Simba B
Huu ndio mpira waliocheza Barcelona kwa muda mrefu tangu wauasisi mwaka 1990, Mlanzi Johan Cruyff akiwemo. Walifanikiwa kuzisumbua timu nyingi za dunia hii. Haikuwa rahisi kuifunga Barca, na kwakuwa wachezaji wengi wa Barcelona walikuwa wanacheza timu ya taifa, wakajikuta wanahamishiwa mfumo huo kwa soka zima la Hispania.
Siku za karibuni, `Tiki-taka football` imekumbana na changamoto. Watu wamejua namba ya kucheza na mfumo huu. Hii inawalazimu Barca na Hispania kukaa chini kuboresha zaidi mpira huu na kuleta mpango B kwasabau huu unaelekeka kushindwa. Si kwamba mpira huu umekwisha, lakini wanatakiwa kuufanyia maboresho.
Ili ufanikiwe kucheza `Tiki-taka football`, moja ya vitu vya kuzingatia ni kuwa na wachezaji ambao wanaweza kucheza nafasi tofauti tofauti uwanjani.
Kwa maana ya mchezaji awe na uwezo wa kusimama nafasi tofauti, ili pale anapotakiwa kuwa beki anatakiwa kufanya hivyo. Na ili kuwapata wachezaji wa aina hii, lazima uwe na akademi za vijana wenye umri tofauti.
Barcelona wana akademi za vijana wa kila aina, wapo 6-10, 10-12, 12-14, 14-16, 16-17, 17-18, na kadhalika. Kwa mfumo huu ni rahisi kumuendeleza mchezaji na kumfundisha nafasi tofauti tofauti uwanjani.
Tiki-taka ni mfumo unaohitaji muda mrefu sana kufikia malengo.
Mkude5Jonas Mkude ni tunda la Simba B
Kaburu wa Simba wakati akiwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo enzi za utawala wa Ismail Aden Rage, alifanya kazi kubwa kuhakikisha Simba ya vijana maarufu kama Simba B inakuwa na mafanikio.
Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Abdallah Matola `Veron`, na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Ibrahim Masoud `Maestro` wakisaidiana na Kaburu walifanikiwa kuzalisha vijana wazuri.
Ramadhan Singano `Messi`, Said Ndemla, Jonas Mkude, Harun Chanongo, Edward Christopher, Wiliam Lucian `Gallas` ni moja ya matunda ya mpango huu makini.
Simba na Azam zimekuwa klabu za mfano kwa soka la vijana. Wengine wanajikongoja, lakini kwa klabu hizi mbili angalau zina mwelekeo ingawa kuna changamoto.
Siku chache zilizopita, Kaburu alisimamia usajili wa wachezaji wawili vijana chini ya miaka 20, Peter Manyika Junior pamoja na beki kinda wa Mwadui ya Shinyanga, Ibrahim Hajibu Migomba.
Baada ya usajili huo, Kaburu alisema malengo ni kuijengga Simba B.
Kwa hili nampongeza Kaburu na wenzake, lakini nadhani imefika wakati wa Simba kuwa na mfumo rasmi wa kupata wachezaji wake.
Kama wanataka kuifanya Simba kuwa klabu bora, lazima viongozi wajikunje kujenga akademi  ya soka la vijana. Lengo liwe ni kuchukua vijana wa umri mdogo zaidi na kukuzwa katika mfumo na utamaduni wa Simba.
Hii itaifanya kuwa klabu ya kisasa. Kwanza wachezaji watakaozalishwa watakuwa wazalendo kwa Simba. Kama mchezaji amekulia katika mazingira ya Simba, lazima aipende klabu yake.
Harun Chanongo (kulia) akiwakimbizi mabeki wa FC Libolo ya Angola kwenye moja ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika. Nyota huyo ni zao la Simba B
Uliona Fabregas, alikuwa Asernal, lakini bado akili ilikuwa Barcelona. Leo hii huwezi kumuondoa, Lionel Messi,  Iniesta, Harnandez katika klabu ya Barcelona. Wamekaa kwa muda mrefu na wanaona utumwa kutoka Katalunya.
Ili kuiga hili,  Kaburu lazima awekeze muda na fedha katika soka la vijana. Inaweza kuwa ngumu kutokana na uwezo wa klabu, lakini naamini Simba ina uwezo wa kufanya hivyo kama nia itakuwepo.
Amini usiamini, mpango huu wa soka la vijana utaibadilisha Simba. Kama Messi, Mkude, Chanongo ni muhimu kwasasa katika timu, basi mafaniko haya yanatakiwa kuwasukumu zaidi kuendeleza soka la vijana.
Kuna haja ya kutafuta utamaduni wa mpira wa Simba ili kuwajenga wachezaji katika mfumo mmoja. Na ili kufanikiwa, lazima pia waamue kuwaamini makocha na kuwapa muda zaidi.
Tafuteni walimu wanaoendana na mpira mtakaobuni katika klabu ya Simba  ili wafanye kazi na vijana wenu kutengeneza mpira rasmi wa Simba.
Leo Milovan, kesho Liewig, keshokutwa kibadeni, mtondo Logarusic. Hapa mtakuwa mnajidanganya tu.
Kaburu kwa hili sina tatizo nawewe, nitakuunga mkono kwa ushauri pia.
- See more at: http://shaffihdauda.com/?p=3434#sthash.U9mirQaQ.dpuf
 
Top