Dili limekamilika: Toni Kroos amethibitisha atajiunga na Real Madrid majira ya kiangazi baada ya kufikia makubaliano binafsi.
LIMEKUWA jambo la faraja kwa Real Madrid baada ya kiungo wa Ujerumani , Toni Kroos kukiri kuwa anaondoka Bayern Munich muda mfupi ujao baada ya kubeba kombe la dunia.
Nyota huyo mwenye miaka 24 alikuwa silaha ya Joachim Low nchini Brazil, hata kama mengi yalikuwa yanazungumzwa kuhusu hatima ya mchezaji huyo.
Na wakati anashangilia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Argentina jana usiku, Kroos alithibitisha kuwa anaweza kujiunga na miamba hiyo ya La Liga.
“Tumemaliza kombe la dunia vizuri sana. Sasa naenda Real Madrid, ni ndoto niliyofanikisha,” Kroos aliwaambia UOL.
Kiungo huyo wa kati anatarajia kulipwa paundi lakini moja na elfu sitini kwa wiki katika dimba la Bernabeu na tayari Bayern Munich imemruhusu kuondoka kwa dau linalokaribia paundi milioni 20.
Kroos amekubali mkataba wa miaka mitano na Carlo Ancelotti, mshindi wa ligi ya mabingwa.
Licha ya kujadiliwa kuwa mchezaji bora kwa miaka ya karibuni barani Ulaya, misimamo yake na mitazamo yake imekuwa ikikosolewa na viongozi wakubwa wa Allianz Arena.
Karl-Heinz Rummenigge na wakurugenzi wenzake walizua maswali baada ya nyota huyo kugoma kupiga penati katika mechi ya fainali ya UEFA dhidi ya Chelsea miaka miwili iliyopita.
Mwanzoni Kroos alikuwa anawindwa na Manchester United chini ya David Moyes, lakini ilishindikana.
Kroos alikuwa katika kiwango bora kwenye fainali za kombe la dunia,na alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Brazil-kitu kilichofanya Louis Van Gaal akodoe macho na kuanza harakati za kumsajili.