Hakuna kitu kibaya kama kutembea na mtu aliyeshiba wakati wewe una njaa. Shibe yake huwa inampa hisia kuwa na wewe umeshiba wakati minyoo inaunguruma ndani ya tumbo lako.
Hekima ya mtu mwenye shibe haimfai mwenye njaa kama hekima ya tajiri isivyomfaa masikini. Katika Dunia yetu mawazo ya tajiri ndio yanamtawala masikini. Hata sheria zote Duniani zimewekwa kwa ajili ya watu wa tabaka la juu kuwatawala watu wa tabaka la chini.
Masikini hua hana thamani wala nafasi ya kusikilizwa katika jamii yetu ya sasa hata biblia takatifu ilishasema kuwa “hekima ya masikini haisikilizwi”. Ndio maana kuna viongozi wachache sana maskini Duniani. Hata viongozi wa masikini ni matajiri, masikini wameshakariri na kukubali bila kujali matokeo hasi yake.
Mfano kwenye bunge letu la Tanzania wawakilishi wa wananchi wa Manzese, Mbagala,T andale wangekua wamevaa uhalisia wa Tandale, Mbagala na manzese kusingekua na bajeti za kuumizana kama hizi.
Ila utakuta mwakilishi wa wananchi wa watu wa Manzese anaishi Osterbay, mwakilishi wa wananchi wa Tandale ana nyumba kubwa Masaki na mwakilishi wa Mbagala makazi yake yapo Msasani, unafikiri hapo kitakachoendelea ni nini, Kama si kiongozi huyo kuhisi maisha yake anayoishi Masaki ni sawa na ya wananchi wake wa Tandale?.
Pamoja na yote hayo kipo kitu kimoja kinachowaunganisha watanzania masikini na matajiri,kitu hicho ni furaha ya tajiri na masikini, shibe ya tajiri na masikini pia haki ya tajiri na masikini.Kiunganishi hicho si kingine bali ni michezo haswa mpira wa miguu.
Mpira wa miguu unadumisha umoja na mshikamano ndani ya nchi yetu.Haswa pale tunapokuwa tunaenda uwanjani kama watanzania tukiwa na lengo na nia moja ya kuishangilia timu yetu ya taifa.
Kaijage nikiwa nimevaa jezi yangu yenye rangi za bendera ya taifa niliyoinunua shilingi 5000 Manzese sokoni huku nikiwa na tiketi yangu ya shilingi 3000 mkononi huku nikiwa nimebaki na shilingi 2000 ya nauli itakayonirudisha nyumbani kwetu Gongo la mboto nikiwa ndani ya uwanja mmoja na Ridhiwani kikwete aliyekata tiketi ya shilingi 50,000 huku naye akiwa amevalia jezi iliyofanana rangi na yangu ila ya kwake ameitoa zizou fassion wote ndani ya uwanja tukiwa na lengo moja tu ya kuishangilia timu yetu ya taifa.
Ni furaha ilioje kuwa na mheshimiwa sehemu moja wote tukiwa tunawaza pamoja huku mioyo yetu ikitamani kitu kimoja.
Sehemu kama hizo ndio sehemu pekee watu wa lika tofauti,matabaka tofauti na nyadifa tofauti tunakutana kwa pamoja tukiwa na lengo moja.
Lakini kuna watu wachache wanaokosa roho za uzalendo wanataka kuharibu umoja wetu pekee uliobaki. Asilimia chache ya warafi wanataka kula raha zote za masikini.Nani asiyejua kuwa nchi yetu ni masikini.?Nani asiyefahamu kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanaishi kwa mlo mmoja? kwa umasikini wetu huo huo tunajibana na kujaza vibubu vyetu tupate shilingi 3000 au 5000 ya kwenda kuishangilia timu yetu ya taifa.
Kwa umasikini wetu na mapenzi ya dhati kwa timu yetu mtu anatembea kwa miguu kutoka Mbeya mpaka Dar es salaam kuja kuishangilia timu yetu ya taifa,Ni mapenzi ya namna gani haya!
Lakini leo TFF ya bwana Malinzi imekuja na kiingilio kima cha chini shilingi 7000,bila shilingi 7000 hakuna kwenda kuiona Taifa stars.Huu ni uonevu kwa watu wa tabaka la chini. Kiwango hiki kitaleta ubaguzi na kuvunja umoja wetu .
Hapa sijui kigezo walichotumia kuweka kiwango hiki lakini kiwango hiki hakiendani na hali ya nchi yetu pia soka letu.Hivi tungekua na kiwango kama cha Nigeria,Misri au Cameroon viingilio vyetu vingekuaje kama kwa mpira huu tu wa kuunga unga kima cha chini cha kiingilio ni shilingi 7000?
Inasikitisha kwakweli,Kiwango hiki kitapunguza idadi ya washabiki watakaoenda uwanjani kuishangilia timu ya taifa,na hamasa uwanjani itapungua.TFF imeangalia faida watakayoipata bila kuangalia hasara itakayowapata.
Sijui ni nani ndani ya shirikisho letu anatoa ushauri kama huu.Unaweza kuweka kiingilio hiki ukakosa vyote.Ukakosa washabiki pia ukakosa fedha ulizotaka kukusanya.Katika pita pita zangu nimeuliza watu 25 wote wamesema hawawezi kulipa shilingi 7000 kwenda kuangalia mechi ya Stars huku wakitoa mawazo kiingilio cha chini kinapaswa kiwe shilingi 5000 au chini ya hapo
Kwa hili TFF imechemka,TFF inapaswa kuzingatia zaidi jinsi gani timu yetu changa itakavyoweza pata matokeo ya ndani ya uwanja bila kujali mapato.Nchi kama Zimbabwe iliweka kiingilio cha dola moja ambayo nia sawa na shilingi 1600 za kitanzania ili kujaza rasilimali watu ndani ya uwanja kuishangilia timu yao ya Taifa.
Lakini TFF yetu imetolea macho mapato ya mlangoni kuliko matokeo ndani ya uwanja.TFF ingeweza kuweka kiingilio cha shilingi 3000 na uwanja wa taifa ukafurika kuishangilia timu yetu changa ya taifa kisha wakapata faida baada ya timu hiyo kufuzu mashindano ya Afrika.
La sivyo TFF itahamishia shilingi 3000 nyingi za watu zilizobidi ziende uwanjani kwenye banda umiza za shilingi 500 kisha 2500 iliyobaki kuimalizia kwa futari kwa mama ntilie.